Jamhuri yapinga maelezo ya shahidi kesi ya Lissu

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 03:48 PM Oct 10 2025
Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Upande wa Jamhuri katika kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu umepinga maelezo ya shahidi wao yawe kielelezo cha utetezi wa mshtakiwa huyo ukidai kwamba hakufuata utaratibu unaotakiwa.

Aidha, Lissu amedai kuwa anaona mawakili wa Serikali wanataka kula keki yao na bado wanataka iendelee, kwa sababu walimpa utaratibu kafuata lakini bado wanapinga.

Hatua hiyo, ilifikiwa na pande zote baada ya Lissu kuliomba Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidizana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde shahidi ambaye ni Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, John Kaaya apewe maelezo yake halisi.

Baada ya kudai hayo, Wakili wa Serikali Mkuu Ajuaye Zegeli amedai kuwa lengo la kutumia maelezo ya shahidi wa Jamhuri ni kuonesha mkinzamo wa kile alichokisema shahidi na alichokiandika.

Amedai kuwa, wakirudi kwenye kesi alizozirejea zile taratibu hajazifuata, kwa mujibu wa hiyo kesi maeneo ya mkinzamo yanapokuwa yameoneshwa ndio anaomba yapokelewe si kusoma upungufu.

"Kwa upande wetu tunaona ameshindwa kuielekeza Mahakama hii vizuri, bado hajamdodosa shahidi kwenye hayo maeneo ambayo ameyaainisha  kwa mujibu wa hiyo kesi,"amedai Wakili Zegeli 

Akiendelea kuunga mkono hoja hizo, Wakili wa Serikali Mkuu Ignas Mwinuka amedai kuwa mshtakiwa hajazingatia ipasavyo kanuni za msingi kwa ajili ya kumhoji shahidi kuaminika kwake.

"Anayepaswa kutoa maelezo hayo kuwa kielelezo ni shahidi, hawajamsikia mshtakiwa akimuuliza shahidi kama anataka kuyatoa badala yake yeye mwenyewe tu ndio ameomba kuyatoa kama kielelezo," Amedai  

Akijibu hoja hizo, Lissu amedai kuwa anaona mawakili wa Serikali wanatala kula keki yao na bado wanataka iendelee,utaratibu wa kuhoji uaminifu wa shahidi umeweka Mahakama ya Rufani katika shauri la Lilian Jesus Fotes na kwenye shauri Shadrack Sospiter.

"Msimamo wa kisheria wa utaratibu hauwekwi na Mahakama Kuu, unawekwa na Mahakama ya Rufani,  uamuzi wa kesi kuhusu suala la kuhoji uaminifu wa shahidi si sahihi," Amedai Lissu

Amedai kwamba katika kesi ya Lilian Jesus Mahakama imesema kwanza maelezo yasomwe, shahidi aelezwe kuwa maelezo yake yanakusudiwa kuhojiwa na kuoneshwa maeneo yenye mkinzano na tatu ni maelezo kupokewa.

"Msimamo wa Mahakama ya Rufani katika shauri hilo huwezi kumdodosa shahidi kabla ya maelezo hayo kupokelewa na kuwa kielelezo. Wahesimiwa majaji msikibali kupelekwa India wakati Sheria zipo hapa, kwa hiyo pingamizi halina msingi na maelezo haya yaingie kwenye kumbukumbu,"Amedai 

Katika suala la kuomba maelezo hayo yapokelewe kama kielelezo, amedai kuwa alimuomba shahidi awasilishe maelezo yake hata kama mawakili wa Serikali hawakusikia. 

Amedai kwamba utaratibu alikuwa haujui, upande wa Jamhuri umemuelekeza na ameufuata utaratibu huo, siku ile alikosea kwa sababu hakuwa na maamuzi hayo, lakini leo aliufuata utaratibu huo.

Akijibu hoja za Lissu,  Wakili Zegeli amedai kuwa baada ya kusikia hoja za mshtakiwa bado msimamo wao ni kwamba utaratibu haujazingatiwa.

Baada ya jopo la majaji kusikiliza hoja hizo, limeahirishwa kesi hiyo hadi Jumatatu saa tatu asubuhi kwa ajili ya kutoa uamuzi huo na kuendelea na maswali ya dodoso.