BURUTE SACCOS yatoa madawati 340 kusaidia shule za Kagera

By Restuta Damian , Nipashe
Published at 04:49 PM Oct 10 2025
Baadhi ya madawati
Picha: Mpigapicha Wetu
Baadhi ya madawati

Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Walimu (BURUTE SACCOS) kimetoa madawati 340 kwa Manispaa ya Bukoba na Halmashauri ya Missenyi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa msingi wa saba wa ushirika — kujali jamii.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mwenyekiti wa BURUTE SACCOS, Charles Tegameisho, amesema wanachama wametenga Shilingi milioni 41.3 kwa ajili ya kutengeneza madawati 340, bima za afya kwa wanafunzi 47 wenye mahitaji maalumu, pamoja na blanketi na pempasi kwa walengwa.

“Hatujanunua tu bila kujua uhitaji, bali tulisikia maombi ya jamii na kuyatekeleza. Bima za afya zitawanufaisha wanafunzi hao kwa mwaka mmoja, popote nchini,” amesema Tegameisho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Jacob Nkwera, amesema manispaa hiyo ina shule za msingi za serikali 26, na inahitaji jumla ya madawati 8,571, huku yaliyopo yakiwa 6,373 na upungufu ukiwa 2,100.

“Kupitia msaada huu, shule kama Kashai, Mafumbo, Tumaini, Kashenge na Rwemishasha zitapata madawati 20 kila moja,” amesema Nkwera.