Serengeti yaitika kwa Samia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:58 PM Oct 10 2025
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan.
Picha: CCM
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan.

Kimbunga, ndilo neno sahihi linaloakisi uhalisia wa maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano mdogo wa kampeni za mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan, wilayani Serengeti mkoani Mara.

Ingawa Dk. Samia amekuwa na rekodi ya kuvutia maelfu ya wananchi katika mikutano yake ya kampeni tangu Agosti 28, lakini kilichotokea katika eneo la Serengeti ni zaidi ya rekodi alizowahi kuziweka.

Inakuwa rekodi kwa sababu kihistoria, eneo hilo aghalabu hunasibishwa na nguvu zaidi ya upinzani. Lakini umati uliohudhuria mkutano mdogo wa Dk. Samia, umeonyesha taswira mbadala na ile iliyozoeleka.

Kilichoshuhudiwa katika mkutano huo sio umati wa wananchi pekee, bali mzuka, shamrashamra na tambo za kila aina zilizoonyeshwa na wahudhuriaji, huku wakiwasilisha ujumbe kuwa Oktoba 29 mwaka huu watajitokeza kwa wingi kupiga kura kumchagua Rais Samia na wagombea wengine wa chama hicho.

Ukiacha rekodi ya umati uliojitokeza, Dk. Samia anavunja rekodi nyingine ya kuwa mgombea urais wa CCM aliyefanya mkutano wa kampeni katika eneo hilo, zikiwa zimepita chaguzi mbili bila mgombea yeyote wa chama hicho kwenda huko.

Mgombea wa mwisho wa CCM kufanya kampeni za urais katika eneo hilo kabla ya Dkt Samia, alikuwa Jakaya Kikwete katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kama ulivyo uhalisia wa haiba ya watu wa eneo hilo, shangilia na shangwe yao, ilikuwa na kila nasaba ya nguvu, uimara na ukakamavu, huku nyimbo za kitamaduni zinazoonyesha nia ya ushiriki wao katika uchaguzi zikisindikiza shamrashamra hizo.