Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameongoza uzinduzi wa programu mpya ya “Konekt Umeme, Pika kwa Umeme” iliyobuniwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), katika viwanja vya Mwembe Yanga, Wilaya ya Temeke.
Programu hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya umeme kwa ajili ya upishi, ikiwa ni hatua ya kupunguza utegemezi wa nishati zenye madhara kwa mazingira na afya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, RC Chalamila amepongeza Wizara ya Nishati, TANESCO na wadau wa maendeleo kwa ubunifu huo unaochochea mapinduzi katika sekta ya nishati nchini.
“Mpango huu ni mwanzo wa zama mpya katika historia ya huduma za umeme nchini. Unauunga mkono kikamilifu juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza matumizi ya nishati safi. Kwa kutumia umeme kupikia, jamii yetu inaelekea kwenye viwango bora zaidi vya maisha,” alisema Chalamila.
Ameongeza kuwa umeme ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na ya taifa kwa ujumla, hivyo kuwekeza katika matumizi yake ni kuwekeza kwenye ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO imetangaza rasmi mpango wa kitaifa wa nishati (Energy Compact) unaolenga kuunganisha wateja milioni 8.5 ifikapo mwaka 2030, sawa na wateja wapya milioni 1.7 kila mwaka.
“Uzinduzi wa programu hii umefanyika kwa wakati muafaka. Kupitia mpango huu, mteja atapatiwa jiko la umeme anapounganishiwa huduma, kisha atalipa kidogo kidogo kupitia mfumo wa token. Hii itarahisisha familia nyingi kutumia umeme kwa kupikia kwa gharama nafuu,” alisisitiza Twange.
Mwisho wa hafla hiyo, RC Chalamila aligawa majiko ya nishati safi ya umeme kwa wananchi mbalimbali na kuwataka kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi katika jamii zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED