Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ametaka jengo la Shule Jumuishi Bahi kukamilishwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kama wadhamini wa ujenzi huo, Benki ya NMB walivyokusudia.
Shule hiyo ya Sekondari Jumuishi inajengwa na Mkandarasi SUMA JKT kwa udhamini wa Benki ya NMB ambao wametoa takribani Sh 4.5 bilioni
Senyamule amesema kiasi kilichotolewa na NMB ni fedha nyingi hivyo lazima matunda yake yaonekana kwani wamewathamini Watanzania wenye mahitaji maalumu ili nao wapate Elimu.
Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza benki ya NMB kwa namna ilivyouheshimisha Mkoa wa Dodoma kwa kujenga majengo mazuri,makubwa na ya kisasa lakini yamejengwa kwa ubora mkubwa unaotakiwa.
"Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan tunawapongeza sana benki ya NMB, wametuheshimisha sana kwani kiasi cha Sh 4.5 bilioni siyo fedha chache, sisi wawakilishi wa Rais tumeridhika na asanteni sana," amesema Senyamule.
Kiongozi huyo amewaagiza wasimamizi wa mradi kutokuwa na kisingizio cha namna yoyote kwani fedha zinatolewa na Taasisi yenye uhakika hivyo akataka jengo likamlike na Januari 2026 watoto waanze kusoma hapo.
Msimamizi wa mradi huo kutoka SUMA JKT Consolata Kajange amesema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 86 na kwamba kazi inakwenda vizuri wakitaraji kumaliza kwa wakati.
Amesema mradi huo wa Shule ya Sekondari Jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji Maalumu Bahi wanaujenga kwa viwango kulingana na mahitaji.
"Utekelezaji wa Mradi ulianza rasmi April 15,2025, Mradi huu unajumuisha ujenzi wa jengo la Utawala 1, Madarasa 6, Maabara 2,Mabweni 2, Jiko na Bwalo 1 na unagharamiwa na Benki ya NMB na utekelezaji wake ni chini ya Mkandarasi SUMA JKT Kanda ya Kati,"amesema Kajange.
Amesema Mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 86 ya utekelezaji kwa ujumla, kwani majengo yote saba yapo katika hatua za mwisho.
Hata hivyo amesema kuna nyongeza ya kazi za ujenzi kama ambayo ni nyumba ya matron na patron 1, ujenzi wa uzio kuzunguka shule mita 940, ujenzi wa chumba cha mlinzi 1 na kupanda miti 600 ndani ya eneo la shule.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kajange, hakuna wanachonyimwa kwa mujibu wa makubaliano na watu wa Benki ya NMB hivyo hawana cha kusingizia kwenye utekelezaji wao akiahidi kukabidhi mradi kwa wakati.
Shule hii sifa yake ya kipekee ni mazingira rafiki kwa mwanafunzi mlemavu kuweza kupata elimu bila changamoto kwani miundombinu yake imekidhi vigezo vyote vya shule jumuishi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED