Upanuzi wa Mgodi wa Shanta Gold kuongeza maisha hadi mwaka 2034

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:08 PM Oct 10 2025
 Upanuzi wa Mgodi wa Shanta Gold kuongeza maisha hadi mwaka 2034
Picha:Mpigapicha Wetu
Upanuzi wa Mgodi wa Shanta Gold kuongeza maisha hadi mwaka 2034

Upanuzi wa shughuli za uchimbaji uliofanyika katika eneo la Porcupine North umeongeza uhai wa Mgodi wa Shanta Gold- New Luika kwa miaka mitano zaidi kutoka mwaka 2029 kufikia 2034. Aidha, kupitia utafiti unaoendelea mgodi huo unatazamia kuongeza zaidi shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu.

Hayo yalibainishwa  na Kaimu Meneja  Mkuu wa Mgodi wa Shanta Gold –New Luika Chunya Mhandisi Ladislaus Kwesigabo,  wakati akizungumza katika mahojiano maalum na timu ya  Madini Diary iliyofika mgodini hapo kwa lengo la kujionea  maendeleo  shughuli za mgodi huo na  namna unavyochangia matokeo chanya ya kiuchumi na kijamii  Wilayani Chunya na taifa kwa ujumla.

Alisema baada ya upanuzi wa eneo hilo shughuli za uzalishaji zinaendelea vizuri na matazamio ni kuendelea na kufanya tafiti zaidi kupitia leseni nyingine zinazomilikiwa na kampuni hiyo ili kuendelea kuongeza uhai wake.

Aprili 3, 2025 Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alizindua shughuli za uchimbaji katika mgodi wa Porcupine North uliopo kata ya Mkola Makongolosi Wilayani Chunya  eneo ambalo linatokana na leseni hodhi  zilizorudishwa  Serikalini kwa mujibu wa Sheria  baada ya kumalizika kwa shauri la kimahakama na mwekezaji wa awali  na hivyo Serikali kuweka utaratibu wa wazi kumpata mwekezaji kuendesha eneo hilo ambapo kampuni ya Shanta ilishinda.

Mgodi wa New Luika unamilikiwa na kampuni ya kitanzania ya Shanta Mining Company Limited. Kampuni ilianzishwa mwaka  2001, mwaka  2004  ilianza kufanya  utafiti wa madini  na mnamo mwaka 2010 ilianza uchimbaji wa madini  na hatimaye  dhahabu ya  kwanza ilianza kuzalishwa mwaka 2012. Tangu mwaka 2012 kampuni ya Shanta imeendela na shughuli za uchimbaji hadi leo ambapo kwa wastani inazalisha wakia 55,000 hadi 60,000 kwa mwaka. 

Mgodi huu  umeajiri watanzania  asilimia 99, asilimia 40 kutoka maeneo yanayozunguka mgodi na asilimia  60 maeneo mengine ya Tanzania huku asilimia 70 ya kampuni za kitanzania zinatoa huduma na bidhaa katika mgodi  huo zikihusisha mitambo  ya kuchimba, usafiri na  huduma nyingine. ‘’ Fursa za kutoa huduma kwenye mgodi yetu zipo na ili ufanye kazi na Shanta uwe umesajiliwa unafanya kazi kihalali na taratibu zetu zinafanyika kwa uwazi,’’ alisema Mhandisi Kwesigabo.

Kuhusu suala la ajira kwa wanawake alisema mgodi huo haujawaacha nyuma kwani umetoa nafasi za ajira kwa wanawake katika fani mbalimbali zikiwemo watafiti, waendesha mitambo, wahandisi na nyingine.

Kuhusu ushiriki wa mgodi huo katika shughuli za kijamii alisema umewekeza katika huduma mbalimbali zikiwemo afya, shule, maji, kilimo pamoja na miradi ya kuwandaa wananchi kuendelea kunufaika pindi mgodi utakapofungwa.

Akizungumzia ukuaji wa shughuli za uchimbaji mdogo Chunya alisema shughuli hizo zinaendelea kukua kwa kasi ukilinganisha na miaka mitano iliyopita na kueleza kwamba, hali hiyo imechochewa na ongezeko la bei ya dhahabu.

Akizungumzia changamoto zilizopo katika uendeshaji wa shughuli za uchimbaji alisema changamoto iliyopo ni baadhi ya wachimbaji wadogo kuingilia baadhi ya maeneo ya leseni za kampuni na leseni za wengine na hivyo kutoa wito kwa wachimbaji wadogo kufuata sheria kwa kutoingilia maeneo ya leseni nyingine.

Uwepo wa mgodi wa New Luika Shanta umeendelea kutoa fursa za kiuchumi na kijamii kupitia ajira, mapato kwa Serikali na kwa mikoa miwili ya Songwe  na Mbeya- Chunya, kupitia miradi mbalimbali inayotokana na  miradi ya (CSR).

Shanta ni mgodi ambao unatekeleza shughuli zake katika maeneo yaliyoshikana, mtambo wa kuchenjua madini upo eneo la Mkoa wa Songwe huku, eneo jipya la uchimbaji baada ya upanuzi la Porcupine North liko katika Wilaya ya Chunya na hivyo maeneo yote yakiendelea kunufaika na uwepo wa mgodi huo. Mbali na mgodi wa New Luika, pia kampuni hiyo inamiliki mgodi wa Singida Gold Mine uliopo mkoani Singida.