Doyo: Nitapunguza misafara ya rais kupunguza matumizi ya Serikali

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 04:32 PM Oct 10 2025
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo.

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amesema iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza nchi atapunguza idadi ya magari yanayokuwepo katika msafari wa rais ili kupunguza gharama kutokana na fedha nyingi kutumika katika msafara huo.

Akizungumza leo (10 Oktoba 2025) na wananchi wa Uyole jijini Mbeya, amesema Watanzania wajiandae kwa mabadiliko makubwa katika utawala wa fedha za Serikali kwani serikali yake itahakikisha inapunguza matumizi mabaya ya fedha hasa kwenye msafara wa magari mengi wa Rais ambao unatumia fedha nyingi za umma.

"Fedha hizi zinapaswa kutumika kwa shughuli za maendeleo ya wananchi, badala ya kuendelea kufadhili msafara wa magari ambayo hayana manufaa kwa watu maskini,"  amesema Doyo na kushangiliwa  na wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Katika kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, Doyo ameweka wazi dhamira yake ya kuleta uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za Serikali, akiamini kwamba ni wakati wa kuwa na serikali inayowajibika kwa wananchi wake.