MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi, amejinadi kinyang’anyiro cha nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika Mashariki kwa kutaja vipaumbele vyake.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Profesa Janabi ameelezea dhamira yake ya kushiriki vyema kujenga Afrika inayojitegemea na yenye afya pamoja na kupambana na vitisho vinavyoikabili ikiwamo vinavyotengenezwa na watu.
Ameelezea uhusiano wa mabadiliko ya tabianchi na afya, uwapo wa magonjwa ya milipuko na kwamba inahitajika mifumo thabiti ili kukabiliana nayo. Kuhusu changamoto amesema utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili unatafutiwa ufumbuzi wa kuifanya Afrika ijitegemee kwenye sekta ya afya.
Akizungumzia vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua, Profesa Janabi amesema inawezekana ipo siku kukawa shwari bila taarifa za kifo na juhudi zinahitajika kuhakikisha mikakati iliyowekwa kwenye Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG 2030) ya kupunguza vifo 70 kati ya 100,000.
Pia, kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kwa asilimia 25. Ameziasa nchi 47 wanachama kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha wanajaribu kufanikisha malengo hayo kwa kuwa yana mafanikio kwa jamii. Profesa Janabi ni mgombea pekee kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Wagombea wengine katika nafasi hiyo ni Profesa Mijiyawa Moustafa (Togo), Dk. Drame Mohamed Lamine (Guinea) na Dk. Nd’a Konan Michael (Ivory Coast), uchaguzi unatarajiwa kufanyika Mei 18, mwaka huu.
Uchaguzi huo unafanywa baada ya aliyeshinda nafasi hiyo Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndungulile, kufariki dunia Novemba, 2024 kabla ya kuanza kuitumikia nafasi hiyo. Dk. Ndugulile aliwahi pia kuwa Waziri wa Afya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED