KATIBU Tawala wa Mkoa wa Manyara, Maryam Muhaji, ameonesha kusikitishwa na kasi ndogo ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto ambavyo vinatolewa na maofisa ustawi wa jamii wa halmashauri.
Muhaji alionesha kusikitishwa na kasi ndogo ya utoaji vyeti vya kuzaliwa jana katika kikao cha mapitio ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM).
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa programu hiyo, iliyosomwa na Ofisa Lishe wa mkoa huo, January Dalushi mkoa ulitoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 20,178 kati ya watoto 46,366 waliozaliwa kwa kipindi cha April hadi Desemba, mwaka jana.
Baada ya kuonekana idadi ya vyeti vilivyotolewa ni ndogo, Katibu Tawala huyo, alimwagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Adam Mandala, kuhakikisha anasimamia hilo mpaka April 30, mwaka huu, watoto wawe wamesajiliwa kwa asilimia 100.
Aidha alisema suala hilo, halikubaliki kusajili watoto kwa kiwango kidogo wakati vitendea kazi vipo na wataalamu walishajengewa uwezo.
"Hili jambo halikubaliki tarehe 30 Aprili mwaka huu nataka nipate taarifa hii, ili kuona hatua gani tumefikia," alisema Muhaji.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Adam Mandala aliahidi kulishughulikia suala hilo.
Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(PJT-MMMAM) mkoani Manyara unatekelezwa na serikali kwa kushirikiana na Shirika la COSITA chini ya mradi wa Mtoto kwanza ambao utatekelezwa mpaka mwaka 2027.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED