Kijiji chafurahia maji wakiyakosa kwa miaka 60

By Daniel Limbe , Nipashe
Published at 04:27 PM Apr 15 2025
Kijiji chafurahia maji wakiyakosa kwa miaka 60
Picha: Daniel Limbe
Kijiji chafurahia maji wakiyakosa kwa miaka 60

WAKAZI wa Kijiji cha Kinsabe, Kata ya Uparamasa, wilayani Chato mkoani Geita, wamepokea kwa shangwe kubwa mradi wa maji safi na salama kutokana na kijiji hicho kutokuwa na huduma hiyo zaidi ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Mradi huo ambao umetekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), umegharimu Sh. milioni 400 na unatarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 7,000.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Louis Bura, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutatua changamoto ya wananchi hao, ikiwamo wanawake na watoto.

Kijiji chafurahia maji wakiyakosa kwa miaka 60
Diwani wa Kata ya Uparamasa, Faustine Mbasa, amesema awali wananchi walikuwa wakinywa maji ya kwenye madimbwi, kwa kuchangia na mifugo pamoja na fisi, hali iliyokuwa ikisababisha kutumia gharama kubwa kujitibia magonjwa yatokanayo na maji machafu.

Chausiku Bomba (65) amesema kupatikana kwa huduma hiyo, kutasaidia kupunguza mimba za umri mdogo kutokana na wanafunzi kukutana na vishawishi vya wanaume wakati wakienda kutafuta maji kwenye vijiji jirani.

Akitoa ufafanuzi Meneja wa RUWASA, wilayani Chato, Avitus Exavel, amesema huduma hiyo ni ukombozi kwa wananchi wa kijiji hicho na kwamba jitihada zinafanyika, ili kuhakikisha vitongoji vyote vitano vya kijiji cha Kinsabe, vinafikiwa na huduma ya maji majumbani pamoja na Ile ya vituo vya kuchotea maji (DP).