Kikwete amhakikishia Samia ushindi wa kishindo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:36 AM Sep 28 2025
Kikwete amhakikishia Samia ushindi wa kishindo
PICHA: CCM
Kikwete amhakikishia Samia ushindi wa kishindo

Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete, amemhakikishia ushindi mgombea urais CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwa hawako tayari kuchanganya pumba na mchele.

Dk. Kikwete ambaye ni Mwenyekiti mstaafu CCM, amesema wanajua madhara yake na hawatodhubutu kufanya hivyo katika uchaguzi mkuu 2025. Dk. Kikwete ameweka wazi hayo leo Septemba 28, 2025, katika mkutano wa kampeni unaoendelea Kibaha.

“Hatuko tayari kuchanganya pumba na mchele katu hatufanyi biashara hiyo tunajua madhara yake,  hatutodhubutu kufanya hivyo. “Ndio maana tunasema Oktoba Tunatiki mara tatu, kwako, wabunge na madiwani,” amesema.

Dk. Kikwete amempongeza Dk Samia kwa kuendelea kuchanja mbuga kusaka kura nchini, akimweleza kuwa kinachomfurahisha ana afya njema.“Umeiongoza nchi vizuri wewe ni mama mwema unajali changamoto za wananchi unaoongoza na mwepesi kuchukua hatua.

“Nchi yetu ina umoja, ina makabila 120 wa rangi mbalimbali waumini wa dini mbalimbali, lakini hakuna ugomvi wa kikabila, rangi wala maeneo, muungano wetu ni imara na bado ni wa mfano barani Afrika na kwingineko.

“Tunashukuru nchi ni tulivu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanaonekana na una maono mazuri kwa miaka mitano ijayo. Tuchague CCM tumchague Dk. Samia aendelee kuongoza,” amewaomba Watanzania.

Dk. Kikwete amemhakikishia Dk. Samia mkoa wa Pwani watamchagua na kumpa kura nyingi zisizo na mfano. “Tutakulipa kura nyingi kwa wema uliotutendea utajaza kura nyingi mpaka zifurike kwenye boksi la kura,” amesema.