MGOMBEA Urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuligeuza zao la bahari, hususan biashara ya dagaa, kuwa sekta rasmi na yenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar.
Akizungumza na wavuvi na waanikaji wa dagaa katika eneo la Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja leo Septemba 28, Othman alisema rasilimali za bahari za Zanzibar zimesalia kuwa wimbo wa kisiasa bila utekelezaji, jambo linalowanyima wananchi fursa ya kufaidika moja kwa moja.
“Dagaa ni biashara kubwa sana inayoweza kuingiza kipato kikubwa kwa wananchi wetu na kusaidia kukuza uchumi wa nchi. Lakini kutokana na mifumo mibovu, wageni ndio wanachukua nafasi huku wavuvi wetu wakiendelea kunyanyaswa,” alisema Othman.
Mgombea huyo aliongeza kuwa Serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha wavuvi na waanikaji wa dagaa wanawekewa mazingira bora ya kufanya kazi zao, ikiwemo mabanda ya kisasa ya uanikaji, miundombinu ya kuhifadhi mazao ya baharini, pamoja na ufuatiliaji wa bei halisi ya bidhaa hiyo katika soko la dunia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED