Samia atimiza mwezi kampeni, atinga Kibaha kwa kishindo leo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:58 AM Sep 28 2025
Samia atimiza mwezi kampeni,  atinga Kibaha kwa kishindo leo
PICHA: CCM
Samia atimiza mwezi kampeni, atinga Kibaha kwa kishindo leo

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ametimiza mwezi mmoja tangu kuzindua rasmi kampeni zake za kusaka urais, ambapo leo ametua Kibaha, mkoani Pwani, kwa kishindo kikubwa.

 Maelfu ya wananchi wamejitokeza uwanja wa CCM  Sabababa, kata ya Mkuza ulioko Picha ya Ndege,  Kibaha, mkoa wa Pwani,  kusikiliza namna atakavyojinadi kwao kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.

Aisha Abdallah na Hassan Ally, wakazi wa Kibaha, wameeleza kuwa Dk. Samia amefanya mambo makubwa yanayombeba awamu ijayo na wako tayari kumpigia kura. “Ameboresha miundombinu ya barabara, maboresho ya sekta ya afya, elimu pamoja na ajira kupitia viwanda vinavyozidi kuibuliwa katika mkoa huu.

“Ameahidi kujenga kongani za viwanda nchini na huku Pwani ndio mahala pale tunavisubiri kwa hamu kubwa kuongeza ajira zaidi,” amesema Aisha. Ally anasema wameshuhudia tofauti, ndani ya miaka minne maisha yamebadilika, huduma zimeboreshwa na heshima ya mkoa huo imeongezeka.