Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wananchi kuwa watulivu na wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kushughulikia changamoto ya usafiri wa Mwendokasi, hususan katika kituo cha Kimara.
Akizungumza katika kituo cha Mwendokasi cha Kimara Mwisho, Chalamila amesema Serikali tayari imechukua hatua madhubuti za kuboresha huduma hiyo. Hatua hizo ni pamoja na kuondoa mtoa huduma wa zamani na kuleta kampuni mpya ambayo imeanza kuingiza zaidi ya mabasi 200 kwa njia ya Morogoro na zaidi ya 150 kwa njia ya Mbagala.
“Ndani ya wiki hii mabasi hayo yataanza kutoa huduma. Tayari yapo ‘yard’-ini yakisubiri kuingizwa barabarani. Tumekutana na kampuni husika na baadhi yataanza kazi muda wowote kuanzia sasa,” amesema Chalamila.
Mabasi hayo mapya yataendeshwa na kampuni binafsi kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuondoa kero zilizokuwa zikiwakabili abiria, hasa wakati wa asubuhi na jioni. Kwa sasa, alisema, mabasi yanayotoa huduma hayazidi 40, jambo lililosababisha usumbufu mkubwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kupitia mitandao ya kijamii.
Mkuu huyo wa Mkoa pia amewataka wananchi kuacha matusi na lawama zisizo na tija dhidi ya viongozi wa Serikali au chama tawala, akisisitiza kuwa Serikali imesikia kilio cha wananchi na hatua madhubuti zinaendelea kuchukuliwa.
“Tumeona clip zinasema hatumtaki mama wala CCM. Nawaomba wananchi tuwe wapole, tusivuruge amani ya nchi yetu. Serikali iko makini, na Rais mwenyewe ameona hali hii na ameagiza hatua zichukuliwe haraka,” amesema.
Mdau mmoja amependekeza magari ya daladala yaruhusiwe kutoa huduma katika baadhi ya maeneo kama Gerezani ili kupunguza adha kwa abiria. Hata hivyo, Chalamila amebainisha kuwa jambo hilo linachunguzwa kwa makini, kwa kuwa kuruhusu daladala kutumia miundombinu ya Mwendokasi kunaweza kuhatarisha usalama kutokana na kutokidhi vigezo vya kiusalama.
Kwa upande wake, abiria mmoja amehoji: kwa nini siasa ziendelee kuingilia mradi huo, na akataka kuona uwekezaji mpya unaoleta matokeo halisi badala ya ahadi zisizotekelezwa.
Chalamila amehitimisha kwa kueleza kuwa mabasi ya Mwendokasi huzalishwa kwa oda maalum kulingana na mahitaji ya eneo husika. Alisisitiza kuwa Serikali iko mbioni kutatua changamoto hiyo na kuwataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED