Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watumishi wa halmashauri nchini kuendelea kujielekeza katika kutatua changamoto za wananchi, huku akiwasisitiza kutumia mapato ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo.
Majaliwa ameyasema hayo leo Wilayani Nzenga Mkoani Tabora wakati akizindua kituo kipya cha mabasi cha Nzega mjini ambacho ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 na kugharimu takribani Sh. bilioni 4.327.
Katika hatua hiyo Waziri Majaliwa pia ameipongeza halmashauri ya Nzega mjini kwa uamuzi wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi, huku akieleza kuwa kitarahisisha huduma za usafiri pamoja na kuibua fursa mpya za biashara kwa wajasiriamali na wakazi wa eneo hilo.
“Kituo hiki ni kizuri na kimejengwa kwa ubora, kinatakiwa kianze kutumika ili wananchi waanze kunufaika nacho, watumishi wa halmashauri ongozeni Wananzega kunufaika na fursa katika eneo lenu.
Pia Majaliwa ametoa wito kwa halmashauri hiyo kuongeza vibanda vya wafanyabiashara badala ya vichache ambavyo vimejengwa mpaka sasa. “Tunataka wananchi wengi zaidi wanufaike, ongezeni vibanda, huu ni ubunifu mzuri sana utasababisha wengi wanufaike, waleteni wajasiriamali hapa wapate riziki zao, mkifanya hivyo mtaongeza mzunguko wa fedha."
Kadhalika, Waziri Majaliwa amesema kuwa serikali inaendelea na mpango kazi wake wa kuwahudumia watanzania wakati wote, “Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kukamilisha malengo yake katika kuwatumikia watanzania ninajua hatua tuliyoifikia”.
Wakati huo huo, Waziri Majaliwa amesema serikali itaendelea kujikita katika utoaji wa huduma muhimu na za uhakika kwa wananchi katika jitihada za kuhakikisha kuwa inakamilisha kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020/25.
Hata hivyo, Majaliwa amewaagiza pia wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa huo kusimama kidete na kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na serikali mkoani humo inakamilika kabla ya Agosti mwaka huu.
Vile vile, amewahimiza wananchi wa Nzega kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na miradi hiyo, ikiwemo kujiunga na huduma ya umeme ambayo tayari imefika kwenye Vijiji vyote 179 na vitongoji 820 vya Wilaya ya Nzega, kama sehemu ya kuunga mkono kampeni ya matumizi ya nishati safi inayosimamiwa na Rais Samia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED