Mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia CCM, Paul Makonda, amesema kuwa mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, anakaa kwenye nafasi hiyo kwa mapenzi ya Mungu na si kwa msaada wa mtu binafsi (‘god father’).
Akihutubia leo, Oktoba 2, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shehe Amri Abeid, Makonda amesema licha ya maneno ya kukatisha tamaa, anaamini Mungu ataendelea kumpa Samia nafasi ya kuongoza nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
“Umekaa hapo kwa mapenzi ya Mungu na atakupa kwa miaka mingine mitano,” amesema Makonda.
Makonda ameongeza kuwa mgombea urais huyo anazunguka mwenyewe kutafuta kura, huku ‘god father’ wake wa kweli wakiwa ni wananchi wenye haki ya kupiga kura.
Aidha, ameiomba serikali ijayo ya Dk. Samia kuhakikisha Arusha inaboresha barabara ili kuhudumia wageni wanaoingia kwa wingi kutokana na ukuaji wa utalii, hasa kupitia filamu The Royal Tour. Pia alisisitiza umuhimu wa kufufuliwa kwa kiwanda cha General Tyre, ili tairi zitengenezwe jijini humo na kuchangia uchumi wa viwanda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED