MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amezindua Kamati ya Maji (Dakio la Mara), huku kamati hiyo ikikabiliwa na jukumu la kutimiza wajibu wa kusimamia rasilimali za maji katika Mkoa wa Mara.
Mtambi amewataka wajumbe walioteuliwa kuongeza bidii katika utekelezaji wa majukumu yao, ili waweze kutimiza kwa uzalendo majukumu ya kuimarisha ulinzi wa raslimali hiyo muhimu kwa maisha ya viumbe hai katika Mkoa wa Mara.
Changamoto mbalimbali zimebainishwa katika hafla hiyo ambapo wadau wa hifadhi ya maji waliomba ushirikiano kutoka ngazi za Mkoa, Wilaya na Halmashauri kushirikiana kutokomeza uvamizi wa vyanzo vya asili vya maji.
Mtambi ameitaka Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), kushirikiana na viongozi wa ngazi za Wilaya, Kata na Vijiji kuchukua hatua kali kwa wanaoingiza mifugo kwenye maeneo ya vyanzo vya maji.
Mtambi ameitaka pia bodi hiyo kufuatilia taarifa za kuwapo kwa shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 za kingo za mto Rubana katika Wilaya ya Serengeti na kuhamasisha utunzaji wa vyanzo vya maji kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akizindua Kamati ya Dakio la Mara, mjini Musoma
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED