Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa, amewataka wananchi kulinda amani na kuepuka maneno yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambayo yanaweza kuvuruga mipango ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza Novemba 20 mjini Mlandizi wakati akipokelewa na wananchi na wanachama waliojitokeza baada ya kuapishwa bungeni, Jumaa alisema hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila kuwepo kwa amani.
“Sisi wenyewe tuna jukumu la kulinda amani yetu. Tutambue bila amani hatuwezi kuishi. Tufanye kazi na tuachane na maneno ya kwenye mitandao,” alisema.
Aidha, Jumaa alisisitiza kuwa chama kiko imara na wanachama hawapaswi kuhofia kuvaa sare za chama kwa kuwa hali ya amani imeimarika zaidi kwa sasa.
Mbunge huyo aliwashukuru wananchi wa Kibaha Vijijini kwa kumuamini na kumchagua, akiahidi kushirikiana na viongozi wa serikali kutekeleza ilani ya chama tawala katika kuwaletea maendeleo.
Akizungumzia hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge, Jumaa amesema imeweka mwelekeo mzuri wa nchi na kupongeza baraza jipya la Mawaziri akiamini litamsaidia Rais kusukuma maendeleo mbele.
Kwa upande wake, Diwani wa Kwala, Mansur Kisebengo, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imepeleka miradi mikubwa katika kata hiyo, huku akiomba maboresho zaidi ya barabara ili kurahisisha usafiri kwa wakazi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED