Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Cameroon, Samuel Eto’o, na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Adebayor, wameonesha nia ya kuja nchini Tanzania kwa ajili ya kukutana na mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, kufuatia tuzo ya Goli Bora la Mwaka Barani Afrika (CAF Goal of the Year 2024/2025) aliyoipokea hivi karibuni jijini Rabat, Morocco.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, muda mfupi baada ya kuwasili nchini akitokea Morocco ambako alienda kupokea kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan tuzo maalum kutoka CAF.
Msigwa amesema Eto’o na Adebayor walivutiwa sana na kiwango cha Mzize na kuonyesha shauku ya kukutana naye, wakimtaja kama mchezaji aliyefanya jambo la kihistoria kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo hiyo kubwa ya CAF.
“Baada ya kusikia Mzize ametangazwa kuchukua tuzo hiyo nilifurahi sana. Niliporudi kukaa, Samuel Eto’o alinifuata na kuniambia akirudi Tanzania anataka kukutana na Mzize. Adebayor naye alisema hivyo hivyo — anataka kuja kumuona na kuzungumza naye,” amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa ushindi wa Mzize ni historia muhimu kwa Taifa, kwani amewashinda wachezaji wengi mahiri barani Afrika, jambo linaloonesha hatua kubwa anazopiga katika mchezo wa soka.
Katika hatua nyingine, Msigwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kutunukiwa tuzo na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kutokana na mchango wake katika kuinua sekta ya michezo nchini.
“Tuzo ya Rais Samia niliikabidhiwa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino. Nilifarijika sana kuona Tanzania inatambulika duniani,” amesema.
Wakati huo huo, Msigwa ametakia heri timu zote za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya kimataifa — Simba, Yanga (Ligi ya Mabingwa Afrika) na Azam FC pamoja na Singida Black Stars (Kombe la Shirikisho). Amesema anatamani kuona angalau timu moja ya Tanzania ikicheza fainali ya michuano hiyo msimu huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED