MGOMBEA Udiwani wa Kata ya Mindu jimbo la Morogoro mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Reuben Sengerema amewaomba wakazi wa kata hiyo kumpa kura za ndio kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 5 mwaka 2026 ili awatatulie changamoto wanazokumbana nazo ikiwemo ukosefu wa mabomba ya maji safi na salama pamoja na kuchelewa kulipwa fidia baada ya kutathminiwa kuhama kwa miaka minne sasa kutoka ndani ya mita 500 kupisha Bwawa la Mindu.
Sengerema amesema hayo leo wakati akifanya kampeni ya nyumba kwa nyumba baada Tume ya taifa ya uchaguzi kutangaza kuanza kampeni za uchaguzi kwenye kata hiyo kutokana na kusitishwa na kutofanyika uchaguzi Oktoba 29 mwaka 2025 baada mmoja wa wagombea wa kata hiyo kufariki dunia.
Akizungumza wakati wa kampeni za nyumba kwa nyumba Mgombea huyo anasema kama wananchi wakimpa ridhaa atasimamia na kutatua changamoto zinazowakumba na kuhakikisha wanaishi kwa kuwa na uhakika wa kukuza uchumi wao.
Mmoja wa wakazi wa mtaa wa Kasanga Kokoto Ally Ligembe (58) ameiomba Serikali kuwasaidia kupata fidia walizoahidiwa ili waweze kwenda kujenga kwenye eneo la Kiegeya walikopewa viwanja na kuendeleza shughuli zao za maendeleo tofauti na walipo sasa ambako wamezuiliwa kufanya shughuli yoyote.
Mmoja wa wazee kwenye mtaa huo mwenye umri wa zaidi ya miaka 80 ambaye hakutaja jina lake anasema wanalazimika kutumia maji ya chemchema licha ya kuwa Jirani na bwawa linalonywesha asilimia 75 ya wakazi wa manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kunywa na matumizi mengine ambapo changamoto ya ukosefu wa mabomba ya maji kwenye eneo hilo ni ya miaka zaidi ya 10 sasa, awali waliwekewa bomba ambalo baada ya muda mfupi lilikatika na halikufanyiwa marekebisho yoyote.
Uchaguzi mdogo unafanyika katika kata mbili za jimbo la Morogoro mjini ambazo ni Mindu na Chamwino kufuatia wagombea wake kufariki dunia ambapo kampeni za uchaguzi huo zimeanzia Oktoba 4 mwaka huu na uchaguzi unatarajia kufanyika Januari 5 mwaka 2026.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED