Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza kuwekwa ndani kwa makandarasi wa kampuni kutoka China ambao wameshindwa kutimiza masharti ya mkataba wa ujenzi wa barabara ingawa Serikali imetimiza wajibu wake kwa kulipa sehemu ya malipo.
Ulega amesema juhudi za kutaka vigogo wa kampuni hiyo kuja nchini na kutoa maelezo kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa barabara waliyopewa kujenga mkoani Dodoma, zimegonga mwamba hadi sasa na sasa kuna uwezekano wa kuwafikisha mahakamani kwa kukiuka masharti ya mkataba.
Kampuni hiyo China First Highway Engineering Co. Ltd imepewa kazi ya ujenzi wa sehemu ya pili ya Barabara ya Ntyuka- Mvumi Hospitali- Kikombo (Km 53) na ingawa tayari imepewa asilimia kumi ya malipo (Sh9.68 bilioni) ujenzi umefikia asilimia mbili.
“Kuanzia sasa hivi, mkandarasi mzembe, mwenye dharau na asiyeendana na ratiba ya mkataba hatutamvumilia na hatua kali za kimkataba zitachukuliwa dhidi yake. Sisi tutaendelea kufanya kazi na kuenzi makandarasi wanaotimiza majukumu yao lakini wale ambao wamepokea fedha zetu lakini hawatimizi upande wao wa mkataba hao tutachukua hatua. Kazi iendelee,” amesema.
Waziri huyo ameagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumshikilia na kumuhoji mkandarasi huyo ambaye alipaswa kufikisha asilimia 13 ya utekelezaji wa mradi huo kufikia sasa hivyo kushindwa kuendana na kasi ya ujenzi licha ya kulipwa fedha kwa wakati.
Aidha, Ulega amesema kuwa licha ya hatua hiyo aliyoichukua pia ataifuatilia miradi mingine inayotekelezwa na mkandarasi huyo na kuahidi kuichukulia hatua zaidi endapo hatoridhishwa na hivyo amemuagiza Naibu Katibu Mkuu, Dk Charles Msonde kuifuatilia kama inaendelea kwa mujibu wa mkataba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED