Baba amuua mtoto wake, ajinyonga baada ya tukio

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 02:29 PM Nov 21 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga
Picha;Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, limethibitisha kuwa mtoto Devina Derick (2), mkazi wa Kijiji cha Isaka, Rungwe, aliuawa kwa kunyongwa na baba yake mzazi, Derick Mwangama (23), kwa kutumia kamba ya manila.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, amesema tukio hilo limetokea Novemba 18, 2025, baada ya mtuhumiwa kumchukua mtoto kwa nguvu kutoka kwa mama yake, Violeth Edward (19), kabla ya kutoweka naye na mwili wa Devina ulipatikana kando ya Mto Kiwira baada ya msako wa wananchi na polisi.

Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa  baada ya mtuhumiwa kutekeleza mauaji ya mwanae  nae alikutwa amejinyonga kwenye mti wa mparachichi karibu na alipotupa mwili wa mtoto.

Kamanda Kuzaga amesema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha tukio ni mgogoro wa kifamilia, amewataka wazazi wenye matatizo kutafuta suluhu kwa njia za kisheria na majadiliano ya amani ili kuepusha madhara kama hayo.