SERIKALI inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila halmashauri nchini inakuwa na kituo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi – VETA – kwa kujenga vyuo vipya na kuboresha miundombinu ya mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana.
Hadi sasa, vyuo 80 vimeanza kutoa huduma na vyuo 65 vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi vikitarajiwa kukamilika mwaka 2026. Akizungumza baada ya kukagua Kazi na bunifu za wanafunzi wa chuo cha VETA Mikumi, mjumbe wa Bodi ya VETA, Abdulhamad Masai, amesema uwekezaji huo ni msingi wa kuzalisha mafundi na wabunifu watakaosaidia taifa kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.
Alisema hatua za ujenzi huo ni sehemu ya mpango mpana wa kujenga jumla ya vyuo 145 kote nchini ambapo wataweka mkazo kwenye fursa ambazo hazikupewa kipaumbele hapo kabla kama alivyoelekeza rais baada ya kuapishwa ikiwemo mafunzo yanayohusu gesi, mafuta,reli ya kisasa na treni ya mwendokasi nk.
Akawahimiza wanafunzi watakaopata mafunzo kutumia fursa za mikopo ya halmashauri kwa kujisajili, kupata leseni na kuanzisha kampuni au biashara zitakazowawezesha kuendeleza ujuzi walioupata.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha VETA Mikumi, Marynurce Kasozi, alisema pamoja na jitihada hizo, bado kuna changamoto za uhaba wa madarasa, maeneo ya mafunzo kwa vitendo na mashine ambazo hazioani na teknolojia ya sasa.
Alisema maboresho ya miundombinu yatawawezesha vijana kupata ujuzi wa kisasa unaohitajika kwenye soko la ajira.Baadhi ya vijana Mariam Temekele wa fani ya ufundi magari na Bahati Mussa wa uchomeleaji waliwahimiza wasichana kuchangamkia fursa ya mafunzo ya ufundi kwa kujiunga na fani za mbalimbali bila hofu.
" Kazi za ufundi zinaweza kufanywa na jinsia zote muhimu ni uaminifu, nidhamu na kujiamini" alisema Bahati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED