Maafisa Usafirishaji, wamachinga kuunda timu kuelimisha amani vijiwe vya bodaboda

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:47 PM Nov 21 2025
Maafisa Usafirishaji, wamachinga kuunda timu kuelimisha amani vijiwe vya bodaboda

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka viongozi wa Maafisa Usafirishaji na Wamachinga kuunda timu maalum itakayozunguka katika vijiwe vya bodaboda na maeneo ya wafanyabiashara kutoa elimu juu ya umuhimu wa kudumisha amani.

Hayo ameyabainisha leo katika kongamano la Maafisa Usafirishaji na Wamachinga wa Wilaya ya Ilala lililofanyika katika Ukumbi wa Drimp Ilala Boma jijini Dar es Salaam, Ambapo Mpogolo amesema amani ni msingi wa maendeleo ya taifa na kila mwananchi anao wajibu wa kuitunza.

Mpogolo ameongeza kuwa bila amani hakuna shughuli yoyote ya kiuchumi inayoweza kustawi, hivyo ni muhimu viongozi hao kuendelea kuwaelimisha vijana na wafanyabiashara juu ya madhara ya vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha ustawi wa wananchi, na juhudi hizo zitafanikiwa zaidi iwapo jamii itashirikiana kulinda amani katika maeneo yote ya jiji.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Wilaya ya Ilala Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi (RPC) ACP. Yustino Mgonja ameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa maeneo mbalimbali kuhakikisha elimu ya kujenga amani inawafikia vijana na makundi yote ya wafanyabiashara pia amesema Jeshi la Polisi litaongeza doria na mikutano ya kijamii ili kuimarisha uhusiano na wananchi. 

Nao viongozi wa Maafisa Usafirishaji na Wamachinga wameahidi kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kutekeleza maelekezo hayo, wakisema watahakikisha wanawafikia bodaboda na wafanyabiashara katika vituo mbalimbali kwa kutoa elimu ya amani kwani ni muhimu kwa sababu sekta ya usafirishaji na biashara ndogondogo ina watu wengi, hivyo kuwa sehemu sahihi ya kuimarisha ushirikiano na ustawi wa jamii.