Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za uchochezi, akiwamo Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Kyela, Victoria Swebe mkazi wa Lubele na wengine watatu ambao ni Bryson Kamembe, Asajile Mwasalemba na Elia Mwalumbu wakazi wa Wilaya ya Kyela.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, SACP Benjamin Kuzaga amethibitisha watu hao kukamatwa kwamba kwa sasa, wanaendelea kuhojiwa huku upelelezi ukiwa katika hatua za mwisho kabla ya taratibu nyingine za kisheria kuchukuliwa dhidi yao pamoja na watu wanaoshirikiana nao.
Siku tatu zimepita tangu taarifa zitolewe katika mitandao ya kijamii kwa nyakati tofauti ikieleza watu hao kukamatwa na watu wasiojulikana.
Katika taarifa nyingine Jeshi la Polisi Mkoa huo, limeeleza kuwa mtoto mwenye umri wa miaka miwili Devina Derick aliuawa kwa kunyongwa kwa kutumia Kamba ya manila na baba yake mzazi Derick Mwangama(23) Mkazi wa Kijiji cha Isaka Wilaya ya Rungwe.
Kamanda Kuzaga amesema tukio hilo limetokea Novemba 18,2025, ambapo mtuhumiwa alifika nyumbani kwa mama wa mtoto, Violeth Edward (19) na kumchukua mtoto kwa nguvu kabla ya kutoweka naye.
Ameeleza kuwa baadae , mwili wa mtoto ulipatikana umetupwa kandokando ya Mto Kiwira na mtuhumiwa Mwangama , naye alijinyonga kwa kutumia kamba ya manila kwenye mti wa mparachichi, karibu na alipotelekeza mwili wa mtoto.
“Uchunguzi wa awali umebaini kwamba chanzo cha tukio hilo ni migogoro wa kifamilia uliokuwepo kati ya wazazi wa mtoto, ambao walikuwa wametengana,” ameeeleza Kamanda Kuzaga.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wazazi na wanandoa wenye migogoro ya kifamilia kutafuta suluhisho kwa njia za kisheria na mazungumzo ya amani, kwa ushirikiano wa ndugu, viongozi wa jamii na wataalamu ili kusaidia kuepusha madhara makubwa kama yaliyotokea.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED