Mgombea urais SAU amwaga sera kwa wananchi Shinyanga

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 05:03 PM Oct 01 2025
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU)Majalio Kyara akinadi sera kwa wananchi wa Shinyanga kwenye mkutano wa kampeni.
Picha: Marco Mduhu
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU)Majalio Kyara akinadi sera kwa wananchi wa Shinyanga kwenye mkutano wa kampeni.

MGOMBEA urais kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara, amenadi sera na Ilani ya chama hicho, kwa wananchi wa Shinyanga, ili wamchague na kuwaletea ukombozi wa maendeleo.

Amenadi sera hizo leo, Oktoba Mosi, 2025 kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Stendi ya Mabasi ya wilaya ya Shinyanga.

Amesema, endapo wananchi watamchagua Oktoba 29, mwaka huu, kwenye Uchaguzi Mkuu, atawaletea maendeleo ya kweli pamoja na kuzalisha ajira milioni 10 kwa mujibu wa ilani ya chama hicho.

“Nawaomba wananchi wa Shinyanga siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, msifanye makosa, bali mnipigie kura nyingi za ushindi na wagombea wote wa ubunge SAU na madiwani, ili tuwaletee ukombozi wa maendeleo,” amesema Kyara.

Amesema, pamoja na ahadi nyingine ataongeza idadi ya machinjio mikoani na vijijini, ili kuongeza thamani ya mifugo na hakuna tena kusafirisha mifugo kwenda jijini Dar es salaam.

Ametaja ahadi nyingine,kuwa ni kushusha bei ya mafuta, ili usafirishaji uwe rahisi, pamoja na Wakulima kusafirisha mazao yao kwa gharama nafuu.