UCHUNGUZI kuhusu matukio ya watu kutoweka umebaini mauaji mapya:
Katika kufuatilia mauaji yanayodaiwa kufanywa na mganga wa kienyeji na wenzake, Jeshi la Polisi limebaini miili mingine 10 ikiwa imefukiwa, baadhi imezikwa kwa mtindo wa kukaa, wakiwamo watoto wa watuhumiwa.
Jeshi la Polisi nchini limefafanua katika orodha hiyo mpya, wawili inadaiwa ni watoto, akiwamo wa mganga wa jadi na wanahisiwa walifukizwa wakiwa hai, matukio hayo yakichukua nafasi katika mikoa ya Singida (3) na Dodoma (7).
Katika mwendelezo wa matukio ya mauaji katika mikoa mitatu kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, alisema jana kuwa miili hiyo 10 ilibainika baada ya mahojiano na watuhumiwa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, liliibuliwa sakata la matukio hayo ya mauaji katika mikoa hiyo ya Dar es Salaam, Tanga na Singida.
Kwa mujibu wa Misime, katika matukio mapya yalibainika mashimo mawili na yaliyofukuliwa na kupatikana mwili wa Gidion Mnyawi, mkazi wa Makuro, mkoani Singida.
Alisema Nkamba Kasubi, aliyemtaja kuwa ni mganga wa kienyeji, anadaiwa alielekeza Mnyawi atolewe kafara kutokana na kuuza shamba kwa watu wawili tofauti, kwa madai kwamba ndio njia ya kurejesha fedha zilizopotea.
DCP Misime alieleza kuwa katika shimo lingine, zilipatikana sehemu za mwili wa binadamu alizozitaja kuwa ni; nyonga, mikono ya kulia na kushoto.
Kamanda huyo alifafanua awali hawakugundua mwenye sehemu hizo za mwili, hata wakalazimika kuchukua hatua za uchunguzi zaidi, akifafanua:
“Baada ya uchunguzi huo na mahojiano ya kina na watuhumiwa ambao ni Selemani Nyalandu, maarufu Hango, Said Msanghaa, maarufu Mangu na Nkamba Kasubi...”
DCP Misime aliendelea: “Walieleza mwili huo ni wa Seleman Idd (23), mkazi wa Makuro Singida, ambaye walimuua kwa kumnyonga na kumfukia katika shimo Juni 23, 2024.
“Askari polisi wataalamu wa ufuatiliaji matukio makubwa walifanikiwa kupata taarifa kuwa kuna mtuhumiwa mwingine ambaye anaitwa Miraji Nyandalu, amehusika katika mauaji haya na wakafanikiwa kumkamata Agosti 25, 2024, huko katika Kijiji cha Misughaa, mkoani Singida.
“Alikuwa anajaribu kutoroka kwa kutumia pikipiki MC 262 CYU, mali ya Daudi Msanku ambaye walimuua na kumzika huko katika Kijiji cha Porobanguma, wilayani Chemba, Dodoma.
“Uchunguzi uliendelea na baada ya mtuhumiwa huyu (Nyandalu) kukamatwa na kukutanishwa na watuhumiwa wenzake, ndipo Nkamba Kasubi, mganga wa kienyeji, Agosti 27, 2024, alikubali kuwaongoza askari polisi hadi katika ‘mji’ (makazi) wake mwingine ulioko Kijiji cha Porobanguma, Tarafa ya Kwamtoro, wilayani Chemba na kuonesha mashimo sita ambayo walifukia watu wengine waliowaua na kuwazika (kuwafukia),” alisimulia.
“Daudi Msanku (27), mkazi wa Gawidu, mkoani Manyara ambaye alipotea Mei 27, 2024, na baada ya kumuua walichoma mwili wake moto kisha majivu yake kuyahifadhi katika ndoo, huyu ndiye ambaye pikipiki yake alikamatwa nayo Nyalandu akijaribu kutoroka baada ya kuona watuhumiwa wenzake wanakamatwa mfululizo na askari polisi," aliongeza.
DCP Misime alisema kuwa baada ya taratibu za ufukuaji kufanyika, ilipatikana miili ya watu wengine aliowataja ni; Seni Jishabi (28), mkazi wa Kijiji cha Porobanguma aliyepotea Machi 3, mwaka huu na watuhumiwa walidai kumuua na kumfukia mwezi uliofuata Aprili 2024.
Mwingine katika orodha ya waliouawa kwa mujibu wa polisi ni; Mohamed Juma (27), mkazi wa Nyamikumbi A, mkoani Singida aliyetoweka tangu Mei 15 mwaka huu ambao watuhumiwa wanadaiwa kumuua kwa kumnyonga kisha kumfukia.
DCP Misime alifafanua namna mauaji hayo yalivyohusisha wanafamilia wa watuhumiwa hao baadhi yao waganga wa kienyeji, akisema: “Ramadhan Yusuph (26), mkazi wa Kidika, mkoani Manyara, ambaye walimuua mwezi Aprili 2024; Mwekwa Kasubi (4), mtoto wa huyo mganga wa kienyeji; aliuawa Machi 2023.
“Maka Nyalandu (2), aliuawa Juni 2023, na ni mtoto wa mtuhumiwa Nyalandu, maarufu Hango. Watoto hawa walizikwa (walifukiwa) wakiwa hai katika zizi la mifugo.
"Pia, watuhumiwa walikiri kumuua Ramadhani Kilesa (80), mkazi wa Porobanguma na kutupa mwili wake katika Pori la Akiba Swangaswanga," alisema DCP Misime, aliyefafanua kuwa mwili wake ulipatikana Julai 25, 2024.
Alisema kuwa awali haikubainika wahusika tajwa wa mauaji yake hadi juzi (Agosti 27) wahusika walipokiri kumuua na kueleza sehemu walipomtupa ili mwili wake "uliwe na wanyamapori", lakini lengo lao halikutimia.
Kugundulika mauaji hayo ya watu 10 katika mikoa ya Singida na Dodoma, DCP Misime alisema unajumuisha utashi na imani hasi katika jamii.
"Hawa wote isipokuwa aliyetupwa katika Pori la Swangaswanga, kwani walibadili mbinu, tisa walizikwa (walifukiwa) kwa kukalishwa katika shimo kwa namna walivyosukumwa na imani zao za kishirikina," alisema.
DCP Misime alisema uchunguzi wa mlolongo wa matukio hayo ya Singida na Dodoma unaendelea, akiahidi polisi itafahamisha umma kadri taarifa mpya zitakapopatikana.
"Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za kweli na sahihi na kuendelea kukemeana kuanzia ngazi ya familia ili kuzuia na kukomesha vitendo hivi vinavyoendelea kutokea ndani ya jamii kwa siri kubwa.
"Kila mmoja wetu tuelimishane kwa dhati, kwa kila mmoja kwa nafasi yake katika jamii ubaya na madhara ya kuendekeza imani za kishirikina, tamaa za mali bila ya kufuata maelekezo ya Mwenyezi Mungu, sheria za nchi na miiko katika jamii, kudhulumiana, kulipiza kisasi na wivu wa mapenzi," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED