TUREJESHE zama zile, jamii ya ushirika Ile jamii ya kale, ya simulizi hakika Tukae muundo ule, mambo kuzungumzika Mimi wewe na jamii, tukuze mazungumzo.
Tuzungumze uwazi, tusife tai shingoni
Lipo jambo huliwezi, liseme usone soni
Wapo wenye na ujuzi, wa jibu la mitihani
Mimi wewe na jamii, tukuze mazungumzo
Pasiwe na wakubaki, kuyaficha maumivu
Na machozi hayatoki, ishara mwenye nguvu ?
Kumbe lipo lipimiki, jambo lipo lilo bovu
Mimi wewe na jamii, tukuze mazungumzo
Tuseme yaliyo ndani, kuyaepusha madhara
Jua umfwate nani, mtu mwenye na busara
Awekaye kifuani, mtunzaji siri bora
Mimi wewe na jamii, tukuze mazungumzo.
Uwepo mara kwa mara, muda wa mazungumzo
Mazungumzo ni dira, na hutoa miongozo
Huzipunguza hasara, nayo mengi matatizo
Mimi wewe na jamii, tukuze mazungumzo
Jamii ijenge moja, nia kushirikiana
Ifanane na daraja, la kuweza kuvushana
Tukikaa kwa pamoja, kubwa huwa dogo sana
Mimi wewe na jamii, tukuze mazungumzo
Tuje afya ya akili, hili tupaze sauti
Tusikwepe kujadili, hata kama hulipati
Tulipe hadhi na hali, nia iwe madhubuti
Mimi wewe na jamii, tukuze mazungumzo
Mshairi: Dk. Raymond Nusura Mgeni, ni daktari wa afya na magonjwa ya akili. Kwa sasa anasomea masomo ya ubingwa eneo hilo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Shirikishi Muhimbili (MUHAS)
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED