Mkuchika aachia Jimbo Newala Mjini

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:43 PM Apr 16 2025
Kapteni Mstaafu George Mkuchika
Picha: Mtandao
Kapteni Mstaafu George Mkuchika

BAADA ya Mbunge wa Newala Mjini, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, kutangaza hatogombea tena ubunge, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, amesema ni watu wachache na waungwana wanapofika wanasema wanapumzika

Ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Shule ya Msingi Butiama, Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara, akimzunguzia mbunge huyo ambaye pia ni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum).

"Mzee Mkuchika amestaafu hivyo wanapaswa kumpata mwenye nguvu ili kusonga mbele. Ni watu wachache na  waungwana wanapofika anasema kupumzika tutaendelea kuchota busara zako ninaamini utatoa ushirikiano," amesema.

Naye, Mkuchika amewahakikishia CCM kuwa jimbo hilo ni la chama hicho.

“Ninataka kushangaa wale wapinzani wanaotaka kuchukua fomu ya ubunge na udiwani. Miaka mitano tutakwenda na Rais Samia Suluhu Hassan na mbunge atakayeteuliwa wakiwamo madiwani,” amesema.

Amewaeleza wana Newala kuna uyoga unaoliwa na usioliwa, akiwataka wasichanganye, waweke unaoliwa kwa nafasi zote.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM, Nape Nnauye, amesema Kapteni Mkuchika, ambaye ni, anastaafu ubunge na kutaka atendewe haki kwa kazi nzuri aliyoifanya Newala.

“Mzee Mkuchika ni Mmakonde halisi ametumia nchi katika nafasi mbalimbali ndani ya CCM, jeshi, serikali, waziri zaidi ya miaka 17 anastaafu bila kashfa.

“Mimi mtoto wa Kimakonde nimelelewa na Mzee Mkuchika nilipokuwa Mkuu wa Wilaya alikuwa Waziri TAMISEMI, mzee anapokwenda kupumzika tumtakie kila la heri. 

“Ni vizuri kuwasemea mema watu wakiwa hai..Mkuchika amekuwa Naibu Katibu Mkuu CCM, lakini kwa vijana ameweka mfano mzuri, ukijua mlango wa kuingilia tafuta mlango wa kutokea kabla watu hawajakutoa

Wewe ni fahari yetu Kusini umeitendea haki,” amesema.

Nape amesema anaamini Mzee Mkuchika hatafunga milango yake, ili waendelee kupata busara zake.