Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Lazaro Jacob Twange, ametoa maagizo kwa mkandarasi wa mradi wa umeme jua kuhakikisha anakamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba.
Amebainisha hayo leo Juni 8,2025 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi wa umeme jua unaotekelezwa katika kijiji cha Ngunga, kata ya Talaga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga. Amesema amesikitishwa kuna mradi huo bado haujakamilika licha ya muda wa mkataba wa awali kuisha.
“Tunamtaka mkandarasi kutekeleza wajibu wake, na sisi kama serikali tutatekeleza wajibu wetu, sisi ndio waajiri, na hatudai bali tunamdai,” amesema Mhandisi Twange. Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Meneja wa mradi huo Emmanuel Anderson, amesema ulianza mwezi Desemba 2023 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Februari 2025,na kwamba Mkandarasi aliomba pia kuongezewa muda wa nyongeza hadi Oktoba mwaka huu.
“Hadi sasa, utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi umefikia asilimia 63. Kiwango cha usanifu ni asilimia 92.7, manunuzi asilimia 78.3, na ujenzi asilimia 54.9,” amesema Anderson. Ametaja gharama za mradi huo kwa awamu ya kwanza kuwa ni sh.bilioni 118 na utazalishwa umeme Megawatt 50.
Mkandarasi wa mradi huo kutoka kampuni ya Sinohydro, Daniel Xu, ametaja changamoto ambazo zilimkwamisha kukamilisha mradi huo ndani ya muda wa mkataba kuwa ni mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana na kuathiri eneo la mradi. Aidha,ameahidi kutekeleza maagizo ya serikali, na kuhakikisha kazi inakamilika kwa muda wa nyongeza waliopatiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED