Waziri Abdallah Ulega: Serikali inatoa kipaumbele cha malipo kwa makandarasi wa ndani

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:50 PM Jun 08 2025
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema serikali inatoa kipaumbele cha malipo kwa makandarasi wa ndani kama mkakati wa kuimarisha uchumi wa taifa na kuendeleza uwezo wa kitaalamu wa wazawa katika sekta ya ujenzi, ambako hadi sasa takribani Sh. Bilioni 90 tayari zimeshalipwa.

Akizungumza leo Juni 8, 2025 mkoani Mwanza katika mjadala kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya ujenzi, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema fedha hizo ni sehemu ya deni la zaidi ya Sh. Bilioni 260, lengo likiwa ni kuhakikisha fedha za miradi ya ujenzi zinarudi nchini.

“Makandarasi wetu wa ndani wakilipwa, uchumi wa nchi unaimarika kwa sababu hela inabaki ndani yetu wenyewe. Rais Samia amenipa maagizo rasmi kuwa kipaumbele cha kwanza kiwe kwa malipo ya makandarasi wetu wa ndani,” amesema Ulega.

Ameeleza kuwa katika muda mfupi tangu kuteuliwa kwake kuongoza Wizara hiyo, tayari wamelipa kiasi hicho kwa utaratibu wa awamu huku takriban Sh. Bilioni 186 zikiwa bado hazijalipwa, huku akitoa hakikisho kuwa serikali itaendelea kulipa madeni hayo hatua kwa hatua kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha.

“Fedha zikipatikana hata kama ni kidogo, cha kwanza ni kuwalipa makandarasi wa ndani. Tunafanya hivi kwa nia ya kulinda uchumi wetu, kuzuia kufilisika kwa makandarasi wetu, na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati,” amesema Ulega.

Amebainisha kuwa, pamoja na changamoto ya madeni mapya kutokana na kazi zinazofanyika kila siku, serikali inajitahidi kuwa na mfumo thabiti wa kulipa madeni hayo bila kuathiri utekelezaji wa miradi mipya.

Kuhusu suala la kutumia wataalamu wa ndani, Ulega amesema serikali inafanya mabadiliko makubwa kuhakikisha wataalamu na kampuni za ndani zinanufaika moja kwa moja na miradi ya ujenzi.