Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Daraja la Kigongo–Busisi ni sehemu muhimu ya kuunganisha miundombinu ya kimkakati inayowezesha usafirishaji wa mizigo kupitia Reli ya Kisasa ya SGR na barabara za mikoa, na hivyo kuongeza tija ya uwekezaji na kukuza uchumi.
Ameyazungumza hayo leo Juni 8, 2025 katika mjadala maalumu unaofanyika mkoani Mwanza kuhusu mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya ujenzi. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mipango ya serikali kufungamanisha miradi ya barabara, reli na bandari ili kuongeza ufanisi wa uchumi wa Kanda ya Ziwa.
“Uwezo wa daraja hili ni wa kipekee katika kuunganisha miundombinu ya SGR ambayo inabeba mzigo mkubwa sana. Kipande cha Mwanza hadi Isaka kimeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 50,” amesema Ulega. Ameongeza kuwa reli hiyo itaunganishwa kutoka Mwanza hadi Tabora, Tabora hadi Dodoma, na kuendelea hadi Kigoma na Msongati, hivyo kuwezesha mtiririko wa usafirishaji wa mizigo kutoka na kwenda kwenye maeneo mbalimbali ya nchi na ukanda wa Maziwa Makuu.
Akizungumzia barabara za kuunganisha daraja hilo, Waziri Ulega amesema tayari serikali imeshampata mkandarasi wa kujenga barabara ya Mwanza hadi Usagara, na kwa sasa wapo kwenye mazungumzo ya kushusha gharama za mradi huo ili kusaini mkataba.
“Nina matumaini makubwa kwamba kabla ya siku ya uzinduzi wa Daraja hili, ambayo itaongozwa na Rais Samia, tutakuwa tumesaini mkataba wa barabara ya Mwanza–Usagara, na mkandarasi ataanza kazi mara moja ili aunganishe na miundombinu ya SGR,” amesema.
Mbali na hilo, serikali inajiandaa pia kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Sengerema–Nyahunge kabla ya Juni 19, mwaka huuambayo itakuwa siku ya uzinduzi rasmi wa daraja hili. Daraja hilo la kimkakati limetajwa kugharimu takriban Sh. bilioni 716, ikiwa ni fedha zote kutoka kwenye kodi za Watanzania kwa asilimia 100, ikijumuisha pia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED