Mpogolo aagiza kufunguliwa barabara Soko Kuu Kariakoo

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 04:09 PM Jun 30 2025
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo akizungumza na wananchi.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo akizungumza na wananchi.

MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amewaagiza wafanyabiashara kufungua barabara zote zinazozunguka Soko kuu la Kariakoo tayari kwa ajili ya uzinduzi ikiwemo na kutaka biashara zote zifanyike ndani ya soko.

DC Mpogolo ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam, alipotembelea soko hilo kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi huo ikiwa na pamoja ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kufungua baraba hizo.

“Ndugu zangu tunakaribia kuzindua soko letu hili ambalo awali lilipata majanga ya kuungua na Rais wetu mpendwa Dk.Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi kuligharamia kulijenga upya hivyo tuwe tayari kulizindua na tufate sheria stahiki bila shuruti kupisha uzinduzi huo” amesisitiza Mpogolo

Amesema wafanyabishara waliozunguka soko hilo ambao wamepanga biashara zao chini na kuweka meza kinyume na utaratibu ndani ya barabara na kupelekea kuzuia magari yasipitae na waendao kwa miguu wakati umefika wa kujipanga vyema na kuachia barabara hizo ziwe wazi na huru zitumike kwa matumizi sahihi.

Amesema moja ya barabara zinazotakiwa ziwe wazi ni pamoja na ile inayoingia sokoni shimoni iwe wazi kuelekea ufunguzi huo. Amesema Soko la Kariakoo ni la Kimataifa na lina matumaini makubwa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi wanaokuja kupata huduma katika soko hilo.

“Jukumu letu ni kuhakikisha Soko liwe na mazingira rafiki litakaloingilika muda wowote barabara zote zinazozunguka soko hilo ziwe wazi na kuhakikisha soko linakuwa safi muda wote lenye kuvutia hatutamvumilia yeyote atakayekaidi maagizo yetu”

“Tutahakikisha wafanyabiashara wote tutawapanga kwa mpangilio  ulio mzuri ili kila amtu anufaike na soko hili”amesema DC Mpogolo. Amesisitiza wafanyabishara wote waingie ndani ya soko ili kuwapa thamani walipa kodi.

DC Mpogolo amesema zoezi la kuwapa elimu wafanyabiashara kujipanga kwa utaratibu limeshaanza kuwaelekeza wachukue hatua ya kujipanga vyema kupisha uzinduzi huo pasipo kusubiri shuruti.