Mtaalamu aeleza tatizo kupoteza kumbukumbu

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:57 AM Jun 11 2024
Mfano wa kichwa unaoonesha ubongo.
Picha: Mtandao
Mfano wa kichwa unaoonesha ubongo.

HIFADHI ya kumbukumbu ya muda mrefu na mfupi katika ubongo ina tatizo ikiwamo kuzongwa na msongo wa mawazo, ‘karani’ anayeshughulika kuhifadhi na kusambaza mafaili hayo hadi kwenye mfumo wa fahamu, atachanganya taarifa.

“Kwenye ubongo kuna sehemu tunaita ‘file clerk’ (karani wa mafaili), ni kama yule mtu ambaye tunamwambia kalete mafaili. Katika ubongo kuna mafaili mengi sana, ila kuna faili ambalo unaliambia nalihitaji hili faili sasa, karani kalibebe...”

Bingwa Mbobezi wa Afya ya Akili na Mfumo wa Fahamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk. Damas Mlaki, amesema hayo akitoa mada kuelimisha umma kuhusu ‘Uhusiano kati ya Kupoteza Kumbukumbu na Afya ya Akili’.

Akifafanua kuhusu aina nne za kumbukumbu katika ubongo, ikiwamo mfumo tumishi yaani karani, ambaye shughuli yake ni kupokea taarifa ya aina gani na faili linalohitajika wakati huo.

“Magonjwa ya akili yanaweza kumkumba mtu na kumsababishia kuchanganya mafaili yaliyohifadhiwa. Sayansi inaonesha kwamba yapo magonjwa ambayo unaweza ukapoteza kumbukumbu za matukio, lakini nyingine zisipotee sana.

“Ili taarifa ziweze kuhifadhiwa kwanza zinasajiliwa kama vile ilivyo masijala na ili usajili lazima milango ya fahamu mitano iwe inafanya kazi, kukiandikisha hicho kitu. Ili uandikishe lazima kiwe kimepelekwa katika eneo la kuhifadhi kumbukumbu za muda mrefu au mfupi.

“Kumbukumbu za muda mrefu, kuna sehemu za ubongo ambazo zinahusika. Kama eneo linahusika lina shida ambalo lina ‘consolidate’ (linaunganisha), ukapita muda unasahau,” anasema Dk. Damas.

Anafafanua kila aina ya kumbukumbu ilivyo na umuhimu, kwa kuwa huhifadhi taarifa na endapo zinahitajika mfumo tumishi (karani), huzifuata katika masijala ya ubongo na kuchukua faili lenye taarifa hizo kwa ufahamu, akisema ni kitendo kinachochukua sekunde chache.

“Mwanasayansi mmoja kila alipokuwa anampa mbwa chakula aligonga kengele na mbwa anakuja huku akiwa anatokwa na udenda. Siku nyingine aligonga kengele, lakini chakula hakumwandalia…

“Mbwa alifikiri ile sauti ndio chakula, mbwa akaja vilevile na udenda, kufika chakula hamna. Maana yake, mbwa alipata hisia kwa kutumia kumbukumbu ya sauti ya kengele na kutokwa na udenda, bila kujali atakikuta chakula au la.”

“Hata kama uliwahi kuadhibiwa hisia zinahifadhiwa, kwa hiyo ukifika au ukitaka kurudia kutenda kosa ambalo lilisababisha ukaadhibiwa hisia zinarudi, unasema hapana, huwezi kutenda tena,” anasema bingwa huyo.

Bingwa mbobezi huyo anasema, ili binadamu awe na uwezo wa kukumbuka, ni lazima karani katika ubongo awe thabiti kwenye mfumo wa kurejea yaliyopita na yaliyohifadhiwa.

Anaeleza kwamba magonjwa yanayoathiri ubongo ni mengi na kumbukumbu za mtu, na kwamba kunahitajika uchunguzi na matibabu kulingana na aina ya kumbukumbu inayopotea.

“Matibabu yapo ya aina tofauti kama vile mlo kamili wenye virutubisho, kulala, ushauri wa kisaikolojia, kujisomea hadithi, kusoma kwenye mitandao ni kuupa mazoezi ubongo, unatulia unapata oksijeni na kumbukumbu kuongezeka,” anasema Dk. Damas.

Dk. Damas ana angalizo kwamba waliothiriwa na magonjwa ya akili kama sonona, muda wa kupona ni chini ya miezi tisa hata kama hawajapewa matibabu, huku akitaja sababu ya kupona ubongo hujitibu kwa mfumo wake wenyewe au kwa kuanzishwa tiba na wataalamu mapema.