Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) imefanya zoezi la kupanda miti rafiki wa maji katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya maji.
Mamlaka hiyo imekuwa ikitekeleza mpango endelevu wa kupanda miti katika maeneo mbalimbali, yakiwemo vyanzo vya maji, maeneo ya matanki ya kuhifadhi maji, na sehemu nyingine zenye uhitaji ili kusaidia kuhifadhi uoto wa asili na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji.
Katika maadhimisho ya mwaka huu, MUWSA imeshirikiana na Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Kilimanjaro, ambako tangi la kuhifadhi maji lipo, kuhakikisha miti inazidi kustawi kwa manufaa ya jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MUWSA, Mhandisi Philbert Nyangwe, ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kushiriki upandaji wa miti ili kusaidia kurejesha uoto wa asili na kulinda vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma, Florah Nguma, amebainisha kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza ofa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ya kurejesha huduma kwa wateja waliositishiwa maji bila faini, endapo watalipia nusu ya deni lao kabla ya tarehe 31 Machi 2025.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa mwaka 2025 yanafanyika kwa kaulimbiu isemayo "Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa Uhakika wa Maji", ikiendelea kuhamasisha umuhimu wa mazingira bora kwa ustawi wa rasilimali za maji nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED