Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema serikali inavuta mitaji kutoka sekta binafsi kwasababu kodi na mikopo hayatoshi kufikia matarajio ya wananchi.
Katika mazungumzo maalum na The Chanzo Machi 29,2025, Kafulila amesema deni la Tanzania ambalo ni Sh. trilioni 97 ni himilivu kwa uchumi wa Tanzania.
Amesema takwimu za Oktoba mwaka 2024 za IMF zilionesha kuwa deni la dunia limefika zaidi ya Dola Marekani trilioni 315 wakati uchumi wa dunia ukiwa Dola trilioni 110 ambako ni mara tatu ya uchumi wa duniani.
Adiha, amefafanua kuwa deni la dunia ndani yake kuna deni la sekta binafsi zaidi ya Dola trilioni 164, deni la kaya ambalo n idola trilioni 48 na deni la serikali trilioni 102 ambalo ni zaidi ya asilimia 90 ya uchumi.
“Kwa Afrika deni la serikali kwa uchumi ni takribani asilimia 57 kwa Tanzania ni takribani asilimia 47, deni linaongezeka ndio lakini ukifanya malinganisho kuna tofauti kubwa kati ya ukuaji wa deni letu kwa uchumi.
“Rwanda deni limefikia asilimia 71 ya uchumi, Kenya 70, Uganda 54, Malawi 84, Msumbiji 76 na Namibia 67,nchi nyingi zinakabiliwa na shida kubwa ya deni lakini sababu kubwa ni serikali kutaka kukidhi matarajio ya watu kwa kuwapa huduma za maji, umeme, afya na Barabara.”
Amesema mahitaji ya wananchi ndio msingi wa madeni kuongezeka jambo linalofanya agenda ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi kuzidi kupata umuhimu kubwa, ili serikali ipunguze majukumu kwenye maeneo ambayo sekta binafsi inaweza kufanya.
Aidha, amesema kwa kushirikisha sekta binafsi mana yake kidogo kinachookolewa na serikali kinatekeleza miradi ambayo sekta binafsi haiwezi kuingia ubia, huku akitolea mfano wa kutoa elimu, lishe na afya kwa kaya maskini ambazo ndio nguzo ya kujenga raslimali watu.
“Raslimali watu ndio sarafu kubwa duniani, ukiwa na watu wengi maskini ukitaka wawe na ubora unahitaji kuwekeza kwenye afya, elimu na lishe yao, sasa utaitoa wapi wakati kidogo hicho ukawekeze kwenye bandari, barabara na reli.Ubia unapunguza ushindani na kuipa nafasi serikali ikawezeke huko ambako hakuna mvuto kwa sekta binafsi kuwekeza,”amefafanua.
Kwa mujibu wa Kafulila, ubia kwenye maeneo ambayo sekta binafsi inaweza kuwa na mvuto kama Barabara, reli. Fedha ambayo ingewekezwa huko inakwenda kwneye huduma za kijamii kwa kuziboresha ili wenye kipato duni kuzipata.
“Ubia unavuta mitaji kutoka sekta binafsi kuweza kuifanya serikali itekeleze miradi bila kutumia fedha yake, ili iokoe hiyo fedha ikaelekezwe maeneo ambayo hayawezi kuwa na mvuto ambayo ni msingi mkubwa kujenga mchumi wenye ushindani na watu wenye ushindani,”amesema.
Kadhalika, amesema mbia akiambia awekeze sehemu isiyo na mvuto kibiashara, hawezi kuwekeza na kwamba atawekeza baada ya kupima na ndio maana hospitali na shule za sekta binafsi zimejengwa maeneo ambayo wananchi watamudu.
“Ila ambao hawana uwezo ni sehemu ya watanzania lazima wapte huduma muhimu kwa wananchi wake, kwa kutumia mtaji wa sekta binafsi inaweza kutekeleza huduma muhimu za kijamii,”amesema.
Amesema ubia ni mkataba wa muda mrefu ambayo mamlaka za serikali zinasaini kwa ajili ya kufanya sekta binafsi itekeleze jukumu lake la kutekeleza miundombinu na huduma mbalimbali.
Lakini serikali inamuita sekta bianfsi kwa mkataba maalum na makubaliano ili atekeleze mradi huo, ambao unakuwa ni ubia kati ya serikali na sekta binafsi ambako kuna mslahi ya pande zote.
“Kwanini tunakuwa na ubia? kuna kwasababu tatu ambazo ni tunataka kuvuta mtaji wa sekta binafsi kufanya majukumu ya serikali, kuvuta teknolojia kwasababu uzoefu unaonyesha sekta binafsi imepiga hatua kuliko serikali, na tatu ni kuleta weledi kwneye menejimenti ambacho kwneye sekta binafsi kipo mbele kuliko serikalini,”amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED