CHAMA cha NCCR Mageuzi, kimewateua Ambar Khamis kupeperusha bendera ya urais huku mgombea mwenza akiwa ni Joseph Selasini katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Wateule hao ambao ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Taifa, na Makamu Mwenyekiti,wamepitishwa Machi 29, mwaka huu katika mkutano mkuu uliofanyika jijini Dodoma na kuwaleta pamoja wanachama wa chama hicho.
Wakizungumza mara baada ya kuteuliwa waliahidi kufanya siasa za kistaarabu kw akulinda tunu za taifa ambazo ni amani, upendo na mshikamano.
Kadhalika wameeleza kwamba watakuwa na sera ya kulinda na kutunza mazingira ili kudhibiti majanga ya mabadiliko ya tabia nchini ambayo yameendelea kuiathiri nchi yetu.
Hadi sasa kati ya vyama 19 vyenye usajili wa kudumu vilivyotangaza na kupitisha wagombea urais wao ni CCM ambao kwenye mkutano maalum mwezi Januari, 2025 walimpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kutetea nafasi ya urais na Makamu wake ni Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Aidha, Rais Hussein Ali Mwinyi alipitishwa kuendelea kutetea nafasi hiyo kwa upande wa Zanzibar.
Machi 20, mwaka huu, Katibu Mkuu wa NLD, Hassan Doyo alitangaza kuwania urais na kuchukua fomu ndani ya chama chake huku akitaja vipaumbele 10 iwapo atapewa ridhaa na watanzania kushika wadhifa huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED