Askari wa usalama barabarani wilayani Igunga mkoani Tabora, WP 8032 PC Victoria aliyeonekana kwenye picha mjongeo akiwa katikati ya wananchi, waliokuwa wakichota mafuta katika ajali ya lori la mafuta anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo kwa kushindwa kuchukua hatua za kiusalama dhidi ya wananchi hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha kukamatwa kwa askari huyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Kamanda Abwao amesema PC Victoria, aliwahi kufika eneo la tukio lakini hakuchukua hatua yoyote kwa watu waliokuwa wakichota mafuta katika ajali hiyo.
Amesema badala yake alionekana kushiriki kwa kutoa dumu kwa raia ili akinge mafuta kinyume na taratimu za ulinzi wa raia na mali zake pamoja na maadili ya kazi ya jeshi hilo.
“Badala ya kuonya wananchi yeye anashiriki hajazinagatia taratibu na maadili ya kazi yetu,” amesema Abwao.
Aidha, Kamanda Abwao amesema ajali hiyo iliyotokana na uzembe wa dereva wa lori hilo lililokuwa na shehena ya mafuta ya dizeli ilitokea Machi 28, 2025 katika Kijiji cha Igogo kwenye barabara kuu ya Igunga-Nzega wilayani humo.
“Dereva wa Lori hilo aligonga kwa nyuma lori lililokuwa limebeba mahindi na baadaye kupoteza uelekeo na kugonga lori jingine ambalo halikuwa na mzigo wowote,”amesema Abwao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED