Ndugai atoa hoja utaratibu kumwona dakatri kwa 10,000/- ufutwe

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 03:23 PM Mar 13 2025
Job Ndugai
Picha: Mtandao
Job Ndugai

SPIKA Mstaafu na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai ameishauri serikali kuangalia upya utaratibu uliopo sasa, katika hospitali nyingi za umma kuwa ni lazima mgonjwa kutoa Sh. 10,000 kwa ajili ya kumuona daktari.

Ndugai, alisema hayo juzi jijini hapa, wakati akichangia hoja kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC), kilichofanyika jijini Dodoma.

Alisema, hivi sasa upo utaratibu ambao unatumika katika hospitali nyingi za umma, kwa wagonjwa kulazimika kutoa kiasi cha Sh. 10,000 ili wamwone Daktari.

“Hivi huu utaratibu wa lazima mgonjwa atoe Sh. 10,000 kwa ajili ya kumwona daktari, nini mantiki yake yaani kumwona mkuu wa mkoa ni bure kumwona waziri ni bure kwanini kumwona dakatari ni Sh. 10,000,” alihoji Ndugai.

Aidha, alisema kama inawezekana utaratibu huo uangaliwe upya, ili kuona viwango hivyo vinapunguzwa kutoa nafuu kwa wagonjwa ambao wamekuwa na uhitaji wa kuwaona madaktari, kwa ajili ya matibabu mbalimbali.

“Mtu anaumwa lakini hawezi kumuona Daktari hadi awe na Sh.10,000, hebu kama inawezekana basi viwango hivi tuone namna ya kuvipunguza ili tutoe unafuu kwa wananchi wanaohitaji kuwaona madaktari,” alisema.

Kadhalika, alisema hivi sasa katika vituo vingi vya afya vilivyopo kwenye maeneo mbalimbali hususani vijiji ambako watu wengi wanatumia huduma ya kadi za bima ya afya ya jamii CHF, wanakosa huduma kutoka na serikali kutorudisha fedha katika vituo hivyo.

“Hivi sasa katika maeneo mengi ya vijijini kule ambako wanatumia sana kadi hizi za CHF, wanalalamika kukosa huduma kutokana na vituo kukosa fedha ambazo serikali ilipaswa kuzirudisha katika vituo hivyo,” alisema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Thomas Rutachunzibwa, akitoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na wajumbe wa kikao hicho, alisema kiasi hicho cha Sh. 10,000 kwa ajili ya kuwaona madaktari kinaenda katika mfuko mkuu wa serikali na siyo mfukoni mwa mtu.

“Fedha hizi zinakwenda kwenye mfuko wa mkuu wa serikali siyo mfukoni mwa daktari, lakini kama ulivyotoa ushauri wako mheshimiwa Ndugai, tutauzingatia kuona namna ya kupitia upya viwango hivi,” alisema Dk. Rutachunzibwa.

Kuhusu fedha zinazopaswa kurudushwa kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kuhudumia watuamiaji wa kadi za Bima ya Afya ya Jamii (CHF), alisema ipo changamoto kidogo ya kimfumo ambayo inafanyiwa kazi na muda siyo mrefu hali hiyo itakua sawa.