CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza rasmi kuhamishia kampeni yake ya ‘No reform, No election’ katika kanda ya Pwani na siku ya kesho wataanzia Kibamba.
Kampeni hiyo itaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, Mjumbe wa Kamati Kuu Godbless Lema, Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Boniface Jacobo, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), Deogratius Mahinyila na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Taifa (BAWACHA), Sharifa Suleiman.
Hatua hiyo, inakuja baada ya chama hicho kutamatisha ziara yake Kanda ya Kusini ambako pia mwenyekiti wa chama hicho akiwa Mbinga, alikamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa mahakamani alikofunguliwa kesi ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Ajenda ya chama hicho ya ‘No reforms, No election’ inalenga kuelimisha wananchi na kuisukuma serikali kubadili mifumo ya uchaguzi, ili kuwapo na haki sawa kwa vyama vyote katika mchakato mzima wa upigaji kura.
Ziara iliyotamatika iliifikia mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa, Songwe, Lindi, Mtwara na Ruvuma.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED