Othman Masoud ajibu hoja za CHADEMA, CHAUMMA kuhusu uchaguzi mkuu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:23 PM May 26 2025
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amejibu hoja kali zilizotolewa na viongozi wa vyama rafiki vya upinzani katika kikao maalum kilichofanyika jana, Mei 25, 2025, mjini Bariadi, mkoani Simiyu. Kikao hicho kilijumuisha viongozi wa ACT Wazalendo na wawakilishi wa vyama vingine vya upinzani kwa lengo la kufafanua msimamo wa ACT Wazalendo kuhusu ushiriki wake katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Katika kikao hicho, Ntemi Jackson Lubelele, Mwekahazina wa CHADEMA Wilaya ya Bariadi, alihoji ni kwa nini ACT Wazalendo haijaungana na CHADEMA katika msimamo wake wa “No Reform No Election” — kauli mbiu inayopinga ushiriki katika uchaguzi bila marekebisho ya msingi ya sheria na tume ya uchaguzi.

Naye, Ngulima Sita, Katibu wa CHAUMMA Mkoa wa Mara, aliitaka ACT Wazalendo kufafanua mbinu itakazotumia kukabiliana na hujuma za CCM, akirejea matukio ya ukiukwaji wa demokrasia katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024.

Othman Masoud: “Tumejifunza, CCM si chama cha kutumikia watu tena — ni biashara ya utajiri wa viongozi”

Akijibu hoja hizo, Ndugu Othman Masoud alieleza kuwa ACT Wazalendo imeamua kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kutokana na uzoefu mkubwa wa kihistoria wa chama hicho kuhusu mbinu za CCM katika kuhujumu mageuzi ya kidemokrasia tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

“Kwa uzoefu wetu, tumejifunza kuwa CCM haitaki kususiwa uchaguzi — wanatumia ususiaji kama fursa ya kujipatia ushindi wa mezani. Sisi tunaamini njia sahihi ni kupambana nao kwa kuhamasisha wananchi wajitokeze na kutumia nguvu yao ya kura.”

Othman alisisitiza kuwa kujitoa kushiriki uchaguzi ni kumwachia CCM uwanja bila mpinzani, jambo ambalo halisaidii maendeleo ya demokrasia nchini.

Mbinu ya ACT: Wananchi ndio “mtaji mkuu” wa mageuzi

Katika kujibu swali kuhusu mbinu za kukabiliana na hujuma, Othman alieleza kuwa mtaji mkubwa wa ACT Wazalendo ni wananchi wenyewe, na jukumu la chama ni kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.

“Sio tu kwamba tunawatumia wananchi kama wapiga kura, bali tunawaandaa kuwa walinzi wa haki yao ya kuchagua. Hatutakubali tena uchaguzi unaoendeshwa kwa mazoea ya hila na vitisho.”