SADC kuondoa vikosi vyake DRC

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:31 PM Mar 13 2025
SADC kuondoa Vikosi vyake DRC
Picha: Mtandao
SADC kuondoa Vikosi vyake DRC

WAKUU wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekubaliana kusitisha zoezi la kutuma vikosi vya kijeshi nchini DR Congo katika mkutano uliofanyika leo Zimbabwe.

Uamuzi huu unahitimisha operesheni ya Umoja wa SADC nchini DRC, iliyokuwa na lengo la kusaidia vikosi vya kijeshi vya Congo kudhibiti hali ya usalama katika mikoa ya Mashariki mwa nchi hiyo.

Katika mkutano huo maalum ulioongozwa na Rais Emmeson Mnangagwa wa Zimbambwe, viongozi wa SADC walionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama inayozidi kuzorota katika mashariki mwa DRC licha yakuwepo kwa vikosi vya kijeshi vya SADC.

Hali hii inajumuisha kutekwa kwa miji muhimu kama Goma na Bukavu, pamoja na kuzuiliwa kwa njia kuu za usambazaji wa misaada ya kibinadamu na kuwa vigumu kufikia wakimbizi wa ndani kwa ndani.

Licha ya uamuzi wa kuondoa vikosi Congo, SADC imesisitiza itaendelea kusaidia serikali ya Jamuhuri ya Congo na kusisitiza kuwa suluhu ya kudumu inahitaji jopo pana la ushirikiano wa kisiasa na kidiplomasia, ambalo litahusisha pande zote, ikiwemo serikali, makundi yasiyo ya kiserikali, na wanamgambo wa M23.

Kuondolewa kwa vikosi vya SADC kumejiri baada ya miaka mingi ya juhudi za kudumisha usalama, ingawa hali ya usalama haionekani kuboreka kwa haraka.

Viongozi wa SADC pia walikumbuka na kutoa heshima kwa wanajeshi waliopoteza maisha wakiwa katika operesheni hiyo, wakituma risala za rambirambi na kuwatakia afueni y aharaka wanajeshi wanaouguza majeraha.

Rais Félix Antoine Tshisekedi wa DRC alieleza shukrani za dhati kwa SADC kwa msaada wake wa muda mrefu katika kukabiliana na changamoto za usalama nchini mwake, huku akikaribisha uamuzi wa kuanza mchakato wa kuondoa vikosi.

Aidha, kikao hicho cha SADC kilitambua uongozi bora wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, ambao walionekana kuwa na mchango mkubwa katika kuratibu ajenda ya amani na usalama katika eneo la SADC.

BBC