Salome Makamba: Kupinga kufanyika Uchaguzi Mkuu ni hatua ya uhaini

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:45 PM Apr 10 2025
Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salome Makamba.

Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salome Makamba, ametoa kauli kali dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, akimtuhumu kwa kuhamasisha vitendo vya "uhaini" kwa kushinikiza kususiwa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Makamba ametoa kauli hiyo leo Aprili 10, bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Amesema kuwa wito wa Lissu wa kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani hadi marekebisho ya sheria ya uchaguzi yafanyike, unakwenda kinyume na misingi ya kidemokrasia, na kwamba siyo njia sahihi ya kushika dola.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzuia uchaguzi ni uhaini. Huyu anataka kutupiga changa la macho. Chama chochote cha siasa duniani, lengo lake la kwanza ni kushika dola. Sasa utawezaje kushika dola kama unagomea uchaguzi?” amesema Makamba.

Aunga Mkono G55, Atangaza Nia ya Kugombea Tena

Mbunge huyo aliongeza kuwa anaungana na kundi la wabunge waliowahi kujulikana kama G55, akieleza dhamira yake ya kugombea tena ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu, ili kuendelea kuwatumikia na kuwatetea wananchi.

Aidha, Makamba ametilia shaka hoja ya "No Reform, No Election", akisema kuwa haiwezi kuwa kigezo cha kuzuia uchaguzi mkuu, kwani mchakato wa marekebisho ya sheria una utaratibu maalum unaojumuisha ushirikishwaji wa wadau.

“Kila mmoja anafahamu mchakato wa utungaji na marekebisho ya sheria ulivyo. Hakiwezi kuwa kisingizio cha kuzuia uchaguzi,” amesema.

“Yeye Ni Nani Hadi Atupangie Nini cha Kufanya?”

Makamba amemkumbusha Tundu Lissu kuwa kama mwanasheria, anafahamu vyema kuwa mabadiliko ya sheria yanahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali na si uamuzi wa mtu mmoja.

“Bahati nzuri yeye ni mwanasheria. Anajua mchakato wa sheria lazima ushirikishe wadau kutoa maoni yao. Sasa leo tumebaki na miezi mitatu kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, anasema hakuna uchaguzi? Hatuwezi kukubali. Yeye ni nani katika nchi hii hadi atupangie nini cha kufanya?” amehoji kwa msisitizo.

Muktadha: Kampeni ya CHADEMA Yazidi Kuzua Mjadala

Tangu kuanza kwa mwaka 2025, CHADEMA kupitia Mwenyekiti wake Tundu Lissu imekuwa ikiendeleza kampeni ya kususia uchaguzi iwapo hakutafanyika mabadiliko ya msingi katika mfumo wa uchaguzi, ikisisitiza “No Reform, No Election”. Kauli hiyo imeendelea kuzua mijadala mikali bungeni na katika jamii kwa ujumla, huku baadhi ya viongozi wakionya kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha ustawi wa kisiasa na amani ya taifa.