Salome Makamba: Tuko tayari kwa Uchaguzi Mkuu 2025, hakuna wa kutuzuia

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 05:00 PM Apr 10 2025
Mbunge wa Viti Maalum, Salome Makamba.

Mbunge wa Viti Maalum, Salome Makamba, amesema kuwa wako tayari kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na hakuna mtu au kundi lolote litakaloweza kuwazuia kushiriki mchakato huo wa kidemokrasia.

Akizungumza leo Aprili 10, 2025, bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Makamba alisema historia inaonesha kuwa vyama vya upinzani vimekuwa vikishiriki uchaguzi mkuu tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

“Uchaguzi wa vyama vingi kwa mara ya kwanza umefanyika mwaka 1995 na tulikuwa na wabunge wa upinzani 51. Mwaka 2000 tulikuwa 26, 2005 tulikuwa 41, 2010 tulikuwa 89, 2015 tulikuwa 116 na mwaka 2020 tulikuwa 28. Katika kipindi chote hicho hakuna mtu aliyewahi kusema kuwa hatushiriki uchaguzi mkuu,” amesema Makamba.

Ameongeza kuwa kauli za kupinga kushiriki uchaguzi ni za kukata tamaa, zinazotolewa na watu wanaoogopa ushindani wa kisiasa.

“Haiwezekani mtu mmoja awe anataka kuamua hatima ya nchi hii peke yake. Mimi ni Salome, msukuma kutoka Shinyanga, sina pa kukimbilia na sitounga mkono mtu anayehamasisha uasi dhidi ya nchi yetu,” amesisitiza.

Akiangazia nafasi ya upinzani katika mfumo wa Bunge, Makamba alisema kuwa kwa sasa hakuna kambi rasmi ya upinzani bungeni, hivyo ni muhimu kwa vyama vya upinzani kushiriki uchaguzi ili kuleta wabunge imara watakaoweza kuikosoa Serikali kwa hoja na kulinda rasilimali za taifa.

“Huwezi kuikosoa Serikali ukiwa nje, lazima uwe ndani. Njia pekee ya kuwa ndani ni kushiriki uchaguzi mkuu 2025. Uanaharakati hautoshi. Kazi ya ubunge siyo ya wanaharakati bali ni ya wawakilishi wa wananchi,” amesema Makamba.