Kuelekea maadhimisho ya Samia Day yanayofanyika kesho katika wilaya zote za Jiji la Dodoma, serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya shilingi trilioni 10 ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Awamu ya Sita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema maadhimisho hayo yataambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali na vikundi vya ngoma, huku yakiendeshwa kwa kauli mbiu "Samia Day – Ametekeleza". Mbiu hiyo inalenga kuonesha mafanikio ya serikali yaliyogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
“Tunaipongeza sana serikali kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika jijini Dodoma, hususan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Maadhimisho haya ni nafasi ya kutangaza mafanikio hayo kwa wananchi,” amesema Senyamule.
Akitaja baadhi ya miradi hiyo, Senyamule amesema serikali imewekeza katika ujenzi wa barabara ya mzunguko (ring road), upanuzi wa vituo vya kuzalisha umeme, maboresho katika sekta ya elimu na afya, pamoja na ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Kwa upande wa nishati, amesema serikali imepanua vituo vya kuzalisha na kusambaza umeme ili kufikia maeneo mengi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na huduma za kijamii.
Akizungumzia maendeleo ya sekta ya elimu, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa mahudhurio ya wanafunzi yameongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na upatikanaji wa chakula shuleni, hali iliyochangia pia kuboreka kwa ufaulu.
“Tumeunda pia timu maalum za kufuatilia kwa karibu masuala ya ufaulu kwa wanafunzi wetu na kuweka mikakati ya kuinua kiwango chao cha elimu kutoka chini hadi juu,” ameongeza.
Senyamule amehitimisha kwa kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo, kwani ni fursa ya kipekee kwao kujionea kazi zinazofanywa na serikali na kushiriki katika mijadala ya maendeleo ya Taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED