Serikali kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi imependekeza kuanzishwa kwa mfumo mpya wa huduma jumuishi wa “one-stop care” utakaochanganya matibabu ya VVU/UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), ikiwemo kisukari na shinikizo la damu. Hatua hii inalenga kuboresha utoaji huduma za afya na kutumia kwa ufanisi zaidi rasilimali zilizopo.
Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu wa wadau wa afya uliofanyika Dar es Salaam, Profesa George Luhago, Mtafiti Mkuu kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), amesema mfumo huo utawezesha wagonjwa kupata huduma zote muhimu kwa ziara moja tu hospitalini.
“Wagonjwa hawatalazimika tena kutembelea kliniki tofauti kwa ajili ya maradhi mbalimbali. Watapimwa, kutibiwa na kufuatiliwa na timu moja ya afya, katika kituo kimoja na kupitia mfumo mmoja,” amesema Prof. Luhago.
Mkutano huo uliwaleta pamoja wadau kujadili namna bora ya kutekeleza mpango huo, kushirikiana matokeo ya tafiti na kuweka mkakati wa pamoja kuhusu upatikanaji wa rasilimali na utoaji huduma.
Mfumo huu wa huduma jumuishi unashirikisha wataalamu kutoka vyuo vikuu vya Harvard na Boston pamoja na mashirika kadhaa ya maendeleo. Moja ya vipengele muhimu ni matumizi ya mfumo wa Activity-Based Costing and Management (ABC/M) unaokadiria gharama halisi za kila huduma, ili kubaini mbinu bora na kuondoa upotevu wa rasilimali.
“Kwa kutumia mfumo huu tunaweza kufuatilia gharama na matokeo ya huduma kwa wakati halisi, hivyo kufanya maamuzi sahihi kuhusu namna bora ya kugawa rasilimali,” ameongeza Prof. Luhago.
Miongoni mwa hatua za awali za utekelezaji ni kuanzisha kliniki zaidi za one-stop nchini, pamoja na kupitia upya sera za ulipaji na viwango vya huduma ili viendane na mfumo mpya.
Kwa upande wake, Dk. Friday Ngaleson, mchumi wa afya, amesema tafiti zinaonyesha kuwa kuunganisha huduma za VVU na NCD hakusababishi gharama kubwa zaidi, bali kunaboresha ufanisi na kuongeza matokeo chanya kwa wagonjwa.
Naye Dk. Kaushal Ramaiya, Rais wa Chama cha Kisukari Tanzania (TDA), amesisitiza kuwa mfumo huo utarahisisha huduma kwa wagonjwa kwani watahudumiwa na mtoa huduma mmoja aliyepewa mafunzo, jambo litakalorahisisha ufuatiliaji na kuongeza ufanisi wa matibabu.
Tanzania bado inakabiliwa na mzigo wa maradhi pacha—VVU/UKIMWI pamoja na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza. Hali hii imeufanya mpango wa huduma shirikishi kuwa wa wakati muafaka na wa kipaumbele.
Wizara ya Afya imesema mfumo huu utaanza kwa majaribio katika mikoa kadhaa kabla ya kusambazwa nchi nzima. Endapo utatekelezwa kwa mafanikio, Tanzania inaweza kuwa kinara barani Afrika katika kuimarisha mfumo wa afya jumuishi, wenye ufanisi na unaomlenga mgonjwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED