Shilingi bilioni 3.39 kuvuna maji ya mvua

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 02:30 PM Mar 13 2025
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usambazaji na Usimamizi wa Mazingira KUWASA, Mhandishi Magige Marwa, akitoa maelezo ya namna ya ujenzi wa chanzo mbadala cha maji yatakayotokana na mvua
Picha: Shaban Njia
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usambazaji na Usimamizi wa Mazingira KUWASA, Mhandishi Magige Marwa, akitoa maelezo ya namna ya ujenzi wa chanzo mbadala cha maji yatakayotokana na mvua

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) mkoani Shinyanga, imeanzisha chanzo mbadala cha maji ya mvua, yanayovunwa katika matangi ya mgodi wa Barrick Buzwagi, yatakayotumika baada ya kutokea hitilafu katika chanzo kikuu cha maji Iherere jijini Mwanza.

Aidha chanzo hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni tatu za maji safi na salama mpaka tangi kuu la maji, linalopatikana eneo la Lunduno, mtaa wa Shunu kata ya Nyahanga Halmashauri ya Manispaa ya Kahama na hatua ya kwanza ya utekelezaji wake imeshakamilika.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usambazaji na Usimamizi wa Mazingira KUWASA, Mhandishi Magige Marwa ameyabainisha haya leo, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji tangu mwaka 2020 mpaka hivi sasa, Mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita, alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maji.

Sh. bilioni 3.39 kuvuna maji ya mvua
Amesema utekelezaji wake umeanza mwezi huu na unatarajia kukamilika Februari mwakani kwa gharama ya Sh. bilioni 3.39 na hatua ya  kwanza ya kununua maungio na kulaza bomba mpaka tangi kuu umeshakamilika na hatua iliyobaki ni utengenezaji wa chujio la maji.

Marwa amesema, maji yamewafikia wananchi 459, 944 katika kata 21 za Manispaa ya Kahama na Msalala kati yake wateja 34,900 wamepata huduma ya maji sawa na asilimia 87 na kwa siku zaidi lita milioni 16 zinatumika na kuwataka wananchi kutunza miundombinu ili iweze kuwanufaisha.

Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Allen Marwa amesema, wamepokea zaidi ya Sh.bilioni tisa kutoka wizara ya maji kwa ajili ya utekelezaji na ukamilishaji wa miradi inayoendelea na ifikapo mwakani, watakuwa na asilimia 96 ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, ameipongeza Mamlaka kwa kuanzisha chanzo mbadala cha maji kitachosaidia kuondoa malalamko kwa wateja wao baada ya chanzo kikuu kuleta shida na kuwataka kukamilisha kwa wakati na kuanza kuwahudumia wananchi.

Amesema, maji yamewafikia wananchi 459,944 kati yake wateja ni 34,900 pekee kutoka kata 21 huku 390,000 wakiwa hawana maji na hao ndio wanaojiunganishia maji kinyemela na kuwataka kutumia wiki ya maji kujitokeza kulasimisha utumiaji wao kabla hatua hazijaanza kuchukuliwa.