SERIKALI imeendelea kulinda na kuboresha ustawi wa wazee nchini kwa kuhakikisha wanapata huduma bora, stahiki na zenye heshima, zinazowawezesha kuishi maisha yenye thamani na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, wakati wa ziara yake katika Makazi ya Wazee Wasiojiweza ya Sukamahela, yaliyoko wilayani Manyoni, mkoani Singida, kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani.
Wakili Mpanju alisema kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wazee katika ujenzi wa taifa, hivyo itaendelea kuwawekea mazingira bora ya kuishi kwa kuhakikisha wanapata huduma za afya, makazi bora na huduma za kijamii kwa ujumla.
"Wazee ni hazina ya maarifa, busara na historia ya taifa letu. Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha hawasahauliki, bali wanapewa huduma bora zitakazowawezesha kuishi kwa furaha, afya na usalama," alisema Wakili Mpanju.
Katika ziara hiyo, Wakili Mpanju alikabidhi zawadi kwa wazee hao kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan. Zawadi hizo ni pamoja na mbuzi, maji safi, mchele, mafuta ya kupikia na televisheni — vyote vikiwa sehemu ya kuhakikisha wazee wanasherehekea kwa furaha na kuendelea kufuatilia matukio muhimu ya kitaifa na kimataifa.
Aidha, alitoa wito kwa jamii na familia kutowatenga wala kuwasahau wazee, bali kuwatambua kama rasilimali muhimu ya kijamii, huku akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha katika masuala ya kisiasa ukiwamo Uchaguzi Mkuu ujao.
"Wazee wetu wana haki ya kupiga kura. Hii ni haki yao ya kikatiba, na ni wajibu wetu kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi wa taifa lao," alisisitiza.
Baadhi ya wazee waliopokea msaada huo walishukuru serikali kwa kuendelea kuwathamini na kuwaenzi, wakisema hatua hiyo imewapa faraja na kuwahamasisha kuendelea kushiriki katika maendeleo ya taifa.
Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani hufanyika kila mwaka Oktoba Mosi, yakiwa na lengo la kutambua mchango wa wazee, kuhamasisha heshima na huduma bora kwa kundi hilo muhimu katika jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED