TANROADS yafunga barabara ya Somanga–Mtama kufuatia mafuriko
By
Mwandishi Wetu
,
Nipashe
Published at 02:57 PM Apr 07 2025
TANROADS yafunga barabara ya Somanga–Mtama kufuatia mafuriko
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi umetangaza kusitisha kwa muda matumizi ya barabara ya Somanga–Mtama, kufuatia mafuriko makubwa yaliyoathiri eneo la barabara hiyo katika Wilaya ya Kilwa, mkoani humo.
Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, na kuharibu sehemu ya barabara ya muda (diversion) inayotumika wakati wa ujenzi wa daraja la Somanga–Mtama.
Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Zengo, amesema kuwa maji yamejaa katika eneo lililoathirika, hali inayofanya barabara hiyo kutopitika kwa sasa.
“Kwa sasa tumeshamjulisha Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, ambaye ameagiza kuchukuliwa hatua za haraka kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara. Ameelekeza barabara ifungwe mara moja ili kutoa fursa kwa wataalamu kuchunguza kiwango cha uharibifu na kuchukua hatua stahiki,” amesema Mhandisi Zengo. 1
Aidha, ameeleza kuwa vifaa vya kazi vipo eneo la tukio na wakandarasi wanaendelea na kazi ya kurekebisha uharibifu huo. Alibainisha kuwa mara tu maji yatakapopungua, shughuli za ukarabati zitaanza mara moja ili kurejesha mawasiliano ya usafiri.
“Maji yakipungua, tutajitahidi kwa haraka kurejesha hali ya kawaida. Tutafungua barabara mara tu itakapokuwa salama kwa matumizi ya wananchi,” ameongeza.
Mhandisi Zengo amesisitiza kuwa usalama wa watumiaji wa barabara ndio kipaumbele kikuu kwa TANROADS, na ndiyo sababu ya kufungwa kwa barabara hiyo kwa muda.
Ametoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa rasmi kupitia mitandao ya kijamii ya TANROADS ili kupata taarifa sahihi na za wakati kuhusu maendeleo ya hali hiyo.