Usiri ni kichaka, kichocheo cha ukatili

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 06:31 PM Oct 01 2025
Mkurugenzi mtendaji wa asasi ya Wanawake katika jitihada za Kimaendeleo Janeth Waminza
PICHA: BEATRICE MOSES
Mkurugenzi mtendaji wa asasi ya Wanawake katika jitihada za Kimaendeleo Janeth Waminza

USIRI umetajwa kuwa kichaka na kichocheo cha kuendelea kutokea kwa matukio ya ukatili hasa wa kijinsia, ambao umesababisha watu kadhaa kupoteza maisha au kupata ulemavu ukiwamo wa kudumu.

Hayo ameyasema Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania(TAMWA) Dk. Roses Reuben kwenye majadiliano yaliyofanyika jana Dar es Salaam kuhusu hali ya ukatili wa kijinsia nchini ulioendeshwa chini ya Mradi wa Sauti zetu. 

“Tumeona baadhi ya watoto wanasema wanaogopa kutoa taarfa za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa kuwa kuna siri za familia, hali ambayo inasababisha wengine wanabakwa, najisiwa na kulawitiwa lakini wanatishiwa, huku wengine wakikubalina ibaki kuwa siri,” alisema.

Dk. Rose alisema ni vyema waandishi  na wanaharakati wakiendelea kujitokeza kupaza sauti kwa njia tofauti ili kuielimisha jamii, kuona umuhimu wa kushiriki kutoa taarifa za manyanyaso au vitisho ili kudhibiti matukio ya kikatili hasa ya kijinsia na kwa watoto.

Mdahalo huo umehusisha baadhi ya wanafunzi kutoka katika shule ya msingi na sekondari ya Mugabe,walimu, wanawake wajasiriamali wa  soko la Mwananyamala, wanaharakati na waandishi wa habari.

Mwezeshaji Frank Sanga anasema waandishi wa habari wamekuwa wakipata madhara hasa ya kisaikolojia wanaporipoti baadhi ya matukio ya ukatili, pia kuna aina ya uandishi unaotumika unakuwa kama kichochoe cha kuongezeka kwa matukio hayo, hivyo vyombo vya habari vinapaswa kutafakari ili kuleta matokeo tofauti katika jamii, ikiwamo kupunguza au kusaidia kukomesha matukio hayo.

Sanga anabainisha mambo kadhaa ambayo yanachochea uwepo wa matukio ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na mauaji kuwa ni afya ya akili, migogoro ya kifamilia wazazi kutendana, ugumu wa maisha, kifo cya mzazi/ wazazi na kumsahau Mungu.

Afisa Ustawi Mwandamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwanayamala Halili Katani anasema kuna umuhimu mkubwa kwa watu wanaofanyiwa ukatili kuripoti matukio hayo haraka kwenye vituo husika, kwa kuwa kuna huduma muhimu hutolewa hasa kwa waliobakwa ikiwamo dawa za kuzuia mimba, pia kuna dawa za kudhibiti maambukizi ya virusi vya ukimwi na iwapo atabainika kuwa tayari ana maambukizi ataanzishiwa dawa.

Anasema maafisa ustawi wamekuwa wakiwapokea na kuwapa msaada wa haraka manusura wanaowakilmbilia kwenye vituo maalum vilivyowekwa, kama ana majeraha ameshindwa kupata fomu namba 3 inayotolewa na polisi, atasaidiwa kupelekwa hospitali kwa matibabu, kisha utaratibu wa kupata fomu hiyo unafanywa.

“Hatua za kisheria ni muhimu kuzingatiwa, lakini kumuokoa manusura ni muhimu zaidi, tunahakikisha usalama wao na kuzingatia wanalindwa kama manusura ni mtoto mdogo hawezi kuhojiwa akiwa pekee yake lazima afisa ustawi wa jamii awepo,” anasema

Mkurugenzi wa asasi ya Wanawake katika jitihada za Kimaendeleo (Wajiki) Janeth Mawinza anasema juhudi za kuzuia matukio ya kikatili hasa ya ubakaji zinapaswa kuongezwa. 

Anasema juhudi hizo ni pamoja na kuelimisha jamii hasa wanaume kuwa walinzi wa watoto mahali popote wanapokuwa kwa kufuatilia nyendo zao na mazingira waliyopo, kama yakiwa hatarishi wasaidie kuwaongoza mahali  salama.